Walimu wa somo la kiswahili wafundwa

 Naibu waziri wa Elimu na Mafunzo ya amali Zanzibar Mmanga Mjengo mjawiri amewataka walimu wa somo la Kiswahili kuanzisha jumuia yao kwa lengo la  kupeana mbinu mbadala za kufundisha somo la Kiswahili kwa wanafunzi.

Naibu waziri wa Elimu ameyasema hayo kufuatia ufaulu mbovu wa wanafunzi kwa somo la kiswahili jambo ambalo linatia aibu kutokana na kiswahili kuwa lugha ya taifa hili.

 Naibu waziri Mmanga ametoa pendekezo hilo leo machi 13, 2018 wakati wa ufunguzi wa semina ya siku moja kwa walimu wa Kiswahili wa skuli za sekondari Unguja sambamba na utoaji wa zawadi kwa washiriki wa shindano la uandishi wa hadithi fupi za kiswahili.

Amesema iwapo walimu wa somo la Kiswahili wataungana na kuanzisha jumuiya yao itasaidia kuondoa vikwazo vinavyopelekea ufaulu mbaya kwa kujadili mbinu itakayosaidia pamoja na kupata misaada mbalimbali kutoka kwa wadau wa kiswahili.

Amesema miongoni mwa makosa yanayofanywa na Walimu hadi kupelekea wanafunzi kushinda kufaulu somo la kiswahili ni pamoja na kasi ndogo ya usomeshaji, kuto kutoa kazi mara kwa mara kwa wanafunzi na uwezo mdogo wa kuwapima wanafunzi wao katika kuwatungia mitihani.

Aidha amesema utafiti unaonesha ufaulu wa somo la Kiswahili upo chini ikilinganishwa na masomo ya sayansi ambayo yanatajwa kuwa na changamoto ya ukosefu wa walimu hivyo ametoa wito kwa walimu hao kutumia mitandao ya kijamii kutafuta mbinu za kufundishia wanafunzi bila kuathiri misingi na tamaduni za lugha hiyo.

Awali akisoma Risala ya baraza la Kiswahili Zanzibar Kaimu Mtendaji wa BAKIZA Omar Adam amesema  licha ya baraza hilo kuendelea  na shughuli za kukuza lugha ya kishwahili lakini wanakabiliwa na tatizo la uhaba wa bajeti na kushindwa  kuendeleza majukumu muhimu ikiwemo kufanya tafiti.

Kaimu Mtendaji wa BAKIZA Omar Adam

Semina hiyo ya siku moja iliyoshirikisha Walimu wa  Skuli za Sekondari  za Unguja, Naibu Mmanga pia amekabidhi zawadi kwa washiriki na washindi wa shindano la hadithi fupi za lugha ya Kiswahili huko katika Ofisi za Baraza hilo Mwanakwerekwe  ili kuongeza hamasa za matumizi ya lugha ya kiswahili Nchi.

Naibu Mmanga pia amekabidhi zawadi kwa washiriki na washindi wa shindano la hadithi fupi za lugha ya Kiswahili huko katika Ofisi za Baraza la kiswahili BAKIZA Mwanakwerekwe