Rais Magufuli aahidi zaidi ya watu laki sita kuajiriwa Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo Machi 14, 2018 amefunguka na kusema kuwa serikali ya awamu ya tano inatatua tatizo la ajira kwa vijana na watanzania kwa vitendo kwani wanatarajia kuajiri zaidi ya watu laki sita.

Magufuli amesema hayo wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi la reli ya kisasa (standard gauge) kutoka Morogoro hadi Makutupora na kusema kwenye ujenzi wa reli hiyo zaidi ya watu elfu thelathini watapata ajira ya moja kwa moja huku zingine zaidi ya laki sita zisizo na moja kwa moja.

Ujenzi wa reli hii ya kisasa unatarajia kutoa ajira thelathini elfu za moja kwa moja na nyingine laki sita zisizo za moja kwa moja zitatolewa wakati wa ujenzi wa reli hii hii itasaidia kupunguza tatizo la ajira nchini vile vile reli hii itasaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira kwa sababu reli hii inatumia umeme” alisema Rais Magufuli

Rais Magufuli amedai kuwa zaidi ya ajira zingine elfu thelathini na tano zinategemewa kutolewa kwenye mradi wa Stigler’s Gorge pamoja na ujenzi wa bomba la mafuta.

Hata hivyo Rais Magufuli amewataka Watanzania kutumia nafasi hizo kwenda kufanya kazi na kuacha kuchagua kazi ili waweze kuingiza pesa na kupata ajira hizo na kudai kuwa mtu ambaye hatafanya kazi hastaili kula na hata akifa ni sawa tu.

“Suala la ajira tunalijibu kwa vitendo, kinachotakiwa kutochagua kazi, hivyo Watanzania mtembee mbele ila mfanye kazi kwani vya bure hakuna asiyefanya kazi asile na asipokula afe tu”alisisitiza Rais Magufuli.