ZSSF imelenga kuleta mabadiliko kwa Wananchi

Mfuko wa Hifadhi ya jamii Zanzibar ZSSF umesema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa Nyumba za Mbweni utaweza kusaidia wananchi wa vipato vya chini na chakati   kumiliki nyumba  za kisasa ambapo pia  itapunguza matumizi holela ya ardhi.

Akizungumza na Zanzibar24  Afisa  Mwandamizi Masoko na Uhusiano kutoka ZSSF Raya Hamdani Khamis amesema hatua za ujenzi wa nyumba hizo  za kisasa zinaendelea vizuri ambapo hadi sasa nyumba zaidi ya 20  zimekamilika na watu wamesha zilipia na wengine wameanza kulipia kidogokidogo.

Amesema  wananchi wa ndani na nje ya nchi  wengi wamekuwa na muamko mkubwa na wengi wamehamasika katika ununuzi wa nyumba hizo zinazojengwa na Mfuko wa hifadhi ya jamii ZSSF.

Bi. Raya amesema lengo kuu la ujenzi wa nyumba hizo za kisasa ni kutaka kuwarahisishia wananchi wa vipato vyote kuweza kumiliki nyumba kwa ajili ya makaazi  pamoja na  kuwaondolea gharama za ujenzi.

Amesema mbali na mradi huo wa ujenzi wa nyumba za Mbweni  kukamilika lakini pia kutakuwaa  na  mradi  mwengine  wa ujenzi  wa  nyumba za kisasa katika eneo la Tunguu kwa ajili ya wananchi wa vipato vya chini zenye bei nafuu ambazo zinakusudiwaa kwa ajili ya wananchi wanyoge.

Aidha amesema mbali na mafanikio  yaliyopatikana katika ujenzi wa nyumba hizo lakini bado mradi unakabiliwa na tatizo upatikanaji wa rasilimali mchanga jambo ambalo limekuwa likizorotesha harakati za ujenzi.

Amesema kupungua kwa rasilimali mchanga Zanzibar imekuwa ni tatizo kwa wakandarasi wengi wa ujenzi  na kupelekea  kununua mchanga kwa gharama kubwa  tofauti na bei  waliyoizoea  hali inayowapa hasara kubwa.

Hata hivyo Afisa Mwandamizi amefafanua kuwa ujenzi wa nyumba za ghorofa  zitaweza kupunguza matumizi mabaya ya ardhi kwani ujenzi wa nyumba kiholela  unasababisha  eneo kubwa kutumika.

Ametoa wito kwa wananchi kuzidisha  mashirikiano  katika hatua zinazochukuliwa na ZSSF  kwani lengo lao ni kutaka kubadilisha maisha ya wananchi na kuleta maendeleo hasa katika kuimarisha mazingira ya makaazi.

Amina Omar