Utafiti: Wasomi wengi hawapendi ajira za utalii

LICHA ya juhudi zinazochukuliwa kuimarisha sekta ya utalii visiwani Zanzibar, imebainika kuwa vijana wengi wanaoajiriwa katika sekta hiyo hawajafikia kiwango cha elimu ya juu ya sekondari kinachohitajika.

Akizungumza katika kikao cha wadau wa utalii kilichofanyika Machi 14, 2018 hoteli ya Marumaru mjini Zanzibar, mshauri mwelekezi wa Jumuiya ya Wawekezaji wa Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI) Selemani Makwita, amesema wengi miongoni mwa waajiriwa wanafanya kazi kwa mazoea kuliko taaluma na ubunifu mpya.

Katika kikao hicho kilichojadili na kupitia utafiti wa ZATI, Makwita alisema miongoni mwa changamoto zinazopunguza idadi ya watu wenye elimu na maarifa yanayohitajika, ni uhakika wa usalama wao kazini na baada ya kumaliza muda wao wa utumishi.

Alisema changamoto nyengine ni mitazamo ya baadhi ya watu kwamba utalii ni sekta isiyofaa kwa dhana kwamba inakwenda kinyume na maadili, tamaduni na miongozo ya imani za kidini.

Aliitaja sababu nyengine inayowafanya watu wengi wenye elimu nzuri kutopenda kufanya kazi kwenye sekta ya utalii, kuwa ni kutokuwepo uhakika wa mustakbali wao wa baadae kuhusiana na mifuko ya ustawi wa jamii kama ilivyo katika sekta ya utumishi wa umma.

Alifahamisha kuwa, matokeo ya utafiti yameonesha kwamba asilimia 81.8 ya waajiriwa wa sekta ya utalii hapa nchini, ni wale wanaofanya kazi katika maeneo yasiyohitaji elimu kubwa wakati asilimia 12.3 ni wenye ujuzi wa wastani.

Aidha alieleza kuwa, asilimia 2.8 tu kati ya watu walioajiriwa katika sekta hiyo ndio wenye kiwango cha kati na cha juu kielimu na ujuzi wa kazi hizo.

“Utafiti pia umezingatia tafauti ya kijiografia na kijinsia ambapo wengi miongoni mwa wafanyakazi wa vijijini na wanawake wanatumika kwenye kazi zisizohitaji ujuzi na taaluma ya juu wakati wachache tu ndio walio kwenye idara za wasomi,” alieleza.

Kwa sababu hizi, alisema watu wenye elimu kubwa wanaona ni vyema kufanya kazi katika sekta nyengine zisizohusiana na utalii ambayo mara nyingi hutoa mikataba ya muda mfupi ambayo  haimuhakikishii mwajirwa hatima yenye mafao mazuri ya baadae.

Akichangia katika mjadala huo, Meneja Rasilimali Watu katika hoteli ya Park Hayyt Bi. Amsi Nyambuche, alisema hoteli zilizoko Zanzibar zinahitaji sana wafanyakazi wazalendo ambao kimsingi ndio walengwa zaidi wa miradi inayowekezwa nchini.

Hata hivyo, alisema kwa kuwa kundi kubwa la vijana wanaopatikana wanakosa hamasa, ni jukumu la waajiri kuwaendeleza zaidi kivitendo, kwa kuwa wanaweza kuwajibika juu ya juhudi walizochukua kuwakuza kitaaluma wafanyakazi wao.

Alisema tatizo la kiwango duni cha elimu na ujuzi kwa vijana wanaobahatika kuajiriwa hotelini, linaweza kupatiwa ufumbuzi iwapo waajiri wataandaa utaratibu maalumu wa kuwaelimisha zaidi ili waweze kuiletea ufanisi taasisi na wao wenyewe.

Aidha alisema ni juu ya wafanyakazi kujituma na kutafuta elimu zaidi itakayowawezesha kupandishwa ngazi na kukabidhiwa idara kubwa na muhimu za kutumikia au hata kuziongoza.

“Kama mtu ameajiriwa ‘house keeping’ (kutunza vyumba), haifai kutosheka na kujiona hana uwezo wa kujiendeleza. Kusoma ndiko kutakakoweza kuwavutia waajiri na kumpandisha ngazi na hivyo kumuongezea kipato,” alisisitiza.

Ofisa kutoka Idara ya Kazi Ameir Ali Ameir, alisema iko haja kwa serikali na taasisi kuhamasisha jamii kubadili mitazamo yao na kuupokea utalii kama mkombozi wa tatizo la uhaba wa ajira nchini.

Alisema bado elimu zaidi inahitajika ili jamii iondokane na mitazamo hasi ili sekta ya utalii iendelee kuwa tegemeo la mapato kwa taifa na wananchi mmoja mmoja.

Mapema, Mwenyekiti wa ZATI Seif Masoud Miskry, alikubaliana na maoni ya wadau hao kwamba kuna haja ya kukutana na Wizara yenye dhamana ya kazi pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kujadili namna ya kuandaa mikakati ya kielimu itakayoamsha ari ya wanafunzi walioko skulini na vyuoni kuchangamkia ajira katika sekta ya utalii.

Alisema wakati Zanzibar inatarajia kupokea kati ya watalii laki sita na saba ifikapo mwaka 2020, lazima kuwe na jitihada za ziada kuwaandaa wafanyakazi wa sekta ya utalii kufanya kazi kwa viwango vinavyokidhi matakwa ya sekta hiyo kikanda na kimataifa.

Na Salum Vuai, MAELEZO.