Upelelezi kesi ya aliyekuwa Rais TFF wakamilika

Baada ya muda mrefu kupita hatimaye upelelezi wa kesi ya kutakatisha fedha inayomkabili aliyekuwa Rais wa shirikisho la soka nchini TFF Jamal Malinzi na wenzake umekamilika.

Mapema leo kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mwendesha mashitaka wa TAKUKURU, Leonard Swai amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Baada ya maelezo ya Swai kwa hakimu Mashauri aliiomba mahakama ipange tarehe kwaajili ya washitakiwa hao kusomewa maelezo ya awali ya upelelezi huo. Malinzi na viongozi wenzake wanatuhumiwa kutakatisha kiasi cha dola za Marekani 375,418.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF katika uongozi wa Malinzi, Mwesigwa Selestine na aliyekuwa Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 28.

Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo na kutaja tarehe ya kusikilizwa tena ambayo ni April 11, 2018 na washitakiwa watasomewa maelezo ya awali. Malinzi na wenzake walikamatwa June mwaka jana na kupandishwa  kizimbani kwa mara ya kwanza June 29,2017.