Ronaldo aonesha rekodi ya kusisimua

Nyota wa Real Madrid Cristiano Ronaldo usiku wa kuamkia leo ameifungia mabao 2 timu yake kwenye ushindi wa mabao 3-0 ilioupata dhidi ya Juventus na kuweka rekodi mbalimbali.

Moja ya rekodi ambayo nyota huyo mwenye miaka 33 ameiweka usiku wa jana ni kuwa mchezaji wa kwanza kufunga katika mechi 10 mfululizo za ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.

Ronaldo pia amefunga mabao 9 dhidi ya Juventus katika mechi 6 alizokutana na timu hizo. Baada ya mabao hayo mawili Ronaldo sasa amekuwa mchezaji mwenye mabao mengi zaidi msimu huu katika mashindano yote akiwa na mabao 39.

Nyota huyo wa Ureno pia ameifikia rekodi ya mlinda mlango wa zamani wa Real Madrid Iker Casilass ya kushinda mechi nyingi zaidi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa ambapo wote sasa wameshinda mechi 95.

Kwa upande wao Juventus wamepoteza mchezo wa kwanza katika dimba lao la nyumbani la Allianz kwenye mashindano ya Ulaya baada ya miaka 5 kupita.