Mambo 4 yakuzingatia kuepuka madhara kipindi cha mvua za Masika

Kama tunavyofahamu kwamba mnamo mwezi wa Machi hadi mwishoni mwa mwezi wa Mei, visiwa vyetu huwa katika msimu wa mvua za Masika.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya Zanzibar imeeleza kuwa mvua hizo zinatarajiwa kuanza kunyesha kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi wa Machi 2018 na kumalizika wiki ya nne ya mwezi wa Mei 2018. Kutokana na mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa, mvua hizo kwa ujumla zitakuwa za wastani hadi juu ya wastani.

Pamoja na taarifa za kiutabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kanda ya Zanzibar kuonesha kuwepo kwa mvua kubwa zitakazoambatana na kimbunga katika kipindi hiki cha mvua za masika hapa Zanzibar, pia uwezekano wa kuongezeka kwa mvua unaweza kuwepo pindipo pakitokea mabadiliko katika mifumo ya joto pamoja na mwenendo wa pepo za pwani. Hivyo, Serikali na wananchi kwa ujumla tunapaswa kuchukua tahadhari ili kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na athari za mvua hizo.

Uzoefu unaonesha kwamba matukio mengi ya kimaafa hujitokeza kila zinaponyesha mvua kubwa. Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na mafuriko, uharibifu wa miundombinu na maradhi ya mripuko ikiwemo kipindupindu na maradhi ya matumbo. Hivyo, ni vyema kwa upande wetu tukachukua hatua za haraka ili kujiweka tayari kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo. Miongoni mwa maeneo ya kuzingatia ni kama ifuatavyo:-

Makaazi:

Uzoefu unaonesha kuwa katika kipindi cha mvua kubwa baadhi ya maeneo hasa katika maeneo ya Mkoa wa Mjini Magharibi hukumbwa na mafuriko na kujaa maji. Hali hii hupelekea familia nyingi kuyahama makaazi yao kwa muda. Hivyo, tunapaswa kusafisha misingi ya kupitishia maji ya mvua katika maeneo tunayoishi, kuhama maeneo ya mabondeni na njia asili za maji na kuhamisha vifaa katika nyumba zilizo katika hatari ya kufikiwa na maji.

Afya ya jamii:
Wakati wa mvua kubwa ambayo huambatana na kujaa na kutuama kwa maji ya mvua, maeneo mengi ya visiwa vyetu hukumbwa na maradhi ya miripuko hasa maradhi ya matumbo na kipindupindu. Chanzo kikuu cha kuzuka kwa maradhi hayo ni kutumia maji yasiyo salama kama vile kutoka kwenye visima au vidimbwi ambayo tayari huwa yamechanganyika na uchafu.
Hivyo wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari kwa kufuata kanuni za afya ikiwemo kuchemsha maji ya kunywa, kutumia dawa za maji zinazotolewa na wataalamu, kufanya usafi binafsi na wa maeneo yanayotuzunguka.

Usafiri:

Kutokana na mvua za Masika zinazotarajiwa kunyesha, baadhi ya maeneo yanaweza kukumbwa na mafuriko yatakayopelekea kuathiri miundo mbinu ya barabara. Aidha, usafiri wa baharini na angani unaweza kuathirika, kwani mara nyingi mvua kubwa huwa zinaambatana na upepo mkali. Hivyo watumiaji wa bahari kama vile wavuvi na wasafiri wanatakiwa kuchukua tahadhari zote. Watumiaji hao wanapaswa kufuatilia mwelekeo wa hali ya hewa kabla hawajafanya maamuzi ya kuendelea na shughuli zao. Sambamba na hilo, Mamlaka husika zinatakiwa kuchukua tahadhari na hatua stahiki ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea katika kipindi hicho.

Miundombinu:

Mvua zikinyesha juu ya wastani kuna uwezekano mkubwa wa kusababisha uharibifu wa miundombinu kama vile uharibifu wa barabara, kukatika au kuanguka kwa nguzo za umeme, kuporomoka kwa milima, kuziba kwa misingi ya kupitishia maji ya mvua na kubomoka kwa madaraja. Kutokana na hali hiyo wananchi wanatakiwa kuepuka kukaa katika maeneo yenye miti mikubwa na nguzo za umeme ambazo zinaweza kuanguka kutokana na upepo au hali ya unyevunyevu ya ardhi na kusababisha nyaya nyingi kuwa wazi. Hali hii inaweza kusababisha matukio ya hatari ambayo mara nyengine hupelekea vifo.

Kutokana na uwezekano wa kutokea athari za mvua hizo, tunazitaka taasisi zote zinazoguswa kwa njia moja au nyengine kuchukua hatua za makusudi ili kujikinga, kujiandaa pamoja na kukabiliana na madhara yoyote yatakayoweza kujitokeza kutokana na athari za mvua hizo.

Hatua pia zinapaswa kuendelea kuchukuliwa na Mabaraza ya Manispaa, Miji na Halmashauri za Wilaya kwa kuzibua misingi ya maji machafu pamoja na kuendeleza na kudumisha usafi wa mazingira. Sote tunafahamu kwamba kazi hii ni ngumu na inahitaji mashirikiano ya pamoja kati ya vyombo hivyo na wananchi.

Serikali inaendelea kuchukuwa hatua mbali mbali za kukabiliana na athari za mvua zinazoweza kujitokeza ikiwa ni pamoja na ujenzi wa misingi mikubwa ya kupitishia maji ya mvua kwa baadhi maeneo yenye kutuama maji kupita Mradi wa Uendelezaji wa Huduma Mjini (ZUSP).

kwa kumalizia, tunawaomba wazazi na walezi kuwasimamia vyema watoto wao wakati wa mvua za Masika zinazotarajiwa kunyesha ili kuepusha majanga ambayo yanaweza kuepukika.

Na Kassim Abdi.