Kocha wa Karume Boys atamba kubeba ubingwa wa CECAFA

Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Zanzibar ya soka chini ya miaka 17 (Karume Boys) Mzee Ali Abdallah amewatoa hofu Wazanzibar juu ya kikosi chao kinachotarajiwa kwenda Burundi katika Mashindano ya CECAFA ya vijana yanayotarajiwa kuanza rasmi April 14 mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kumaliza mazoezi mchana wa leo katika uwanja wa Amaan Kocha Mzee amesema wameamua kufanya mazoezi mchana ili kuzowea mazingira ya Burundi katika Mashindano hayo kwani katika ratiba wamepangiwa kucheza michezo mengine mchana huku akiwatoa hofu wa Wazanzibar na kusema kuwa anaamini kikosi chake kitatwaa Ubingwa wa Mashindano hayo.

“Tunashukuru Mungu mazoezi yanaendelea vizuri mana Vijana wanapokea vizuri mazoezi, tumeamua kufanya mazoezi mchana kwasababu kule Burundi ratiba ya michezo yetu siku nyengine tunacheza mchana ili tuzowee mazingira, mimi naamini vijana hawa kwa vile wanaari kubwa watabeba ubingwa na Wazanzibar wasiwe na wasi wasi wowote”.

Aidha kocha Mzee amesema hana wasi wasi kwa timu zilizomo katika kundi lao B huku akisema wao wanaamini watashinda bila ya woga wowote.

“Baadhi ya watu wanasema kundi letu B ni kundi la Kifo lakini mimi sina wasi wasi wowote wa timu zile, sisi tunajivunia vipaji na vijana wanahamasa ya kufanya vyema kama kaka zao Zanzibar Heroes”. Alisema Kocha Mzee.

Wakati huo huo kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) na Msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Hemed Suleiman (Morocco) amesema Zanzibar ina vipaji vingi hivyo anaamini kikosi cha Karume Boys kitafika mbali katika Mashindano hayo.

“Mimi sina wasi wasi na vijana hawa kwasababu tuna program nzuri ya Vijana na pia tuna vipaji, japo tumecherewa kuanza mazoezi na vijana hawa lakini watafika mbali”. Alisema Kocha Morocco.

Mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi nchini Burundi April 14 hadi 28, 2018 ambapo Zanzibar imepangwa kundi ‘B’ pamoja na ndugu zao Tanzania bara, Sudan na Uganda huku kampeni zake Zanzibar kuwania kombe hilo zitaanza kwa kucheza na Sudan April 15 katika uwanja wa Gitega majira ya saa 7:30 za mchana.

 

Na Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.