Chanzo na dalili za ugonjwa wa Saratani ya shingo ya kizazi

Serikali ya Tanzania imezindua kampeni ya chanjo ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi ambapo zaidi ya wasichana laki 6 walio na umri kati ya miaka 9 hadi 14 watachanjwa nchi nzima.

Duniani, kuna zaidi ya wanawake 260,000 wanaofariki kwa sababu ya saratani ya shingo ya kizazi

 

 

Serikali ina matumaini kuwa kampeni hiyo itapunguza gharama za afya. Kumuuguza mgonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi kunaweza kugharimu takriban dola za Marekani elfu 2 wakati dola 15 zitatumika kuwachanja wasichana maafisa walisema.

SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI NI NINI?

Saratani ya shingo ya kizazi ni aina ya saratani inayotokea katika chembechembe za shingo ya kizazi, ambayo ni sehemu ya chini ya mji wa mimba (uteri) inayoungana na uke. Aina mbalimbali za virusi aina ya papilloma wamethibitishwa kusababisha saratani hii ambayo hujitokeza kwa wingi miongoni mwa wanawake duniani kote, hususani wenye umri kati ya  miaka 20 na 39.

Saratani ya shingo ya kizazi ni ya pili miongoni mwa saratani zinazowapata wanawake ambapo wagonjwa wapya wapatao 529,828 hugunduliwa kila mwaka, 85% wakiwa ni katika nchi zinazoendelea. Inabakia kuwa ya pili baada ya saratani ya matiti kwa kusababisha vifo vitokanavyo na saratani, ambapo huchangia 10% ya vifo vitokanavyo na saratani mbalimbali kwa wanawake. Inakadiriwa kuwa zaidi ya wanawake 275,000 hufa kila mwaka kwa ugonjwa huu, idadi kubwa ni kutoka nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

AINA ZA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI.

Kuna aina mbili za seli kwenye shingo ya kizazi (cervix) ambazo ni squamous cell na glandular calls, hivo saratani ambayo huanzia kwenye seli za squamous huitwa “squamous cell carcinoma” na saratani inayoanzia kwenye seli za glandular huitwa “adenocarcinoma”. Jambo muhimu la kufahamu ni kwamba Saratani inapoanza huwa ni vigumu sana kuigundua kwani haioneshi dalili zozote, hivo unaweza usigundue mpaka pale saratani imefikia hatua mbaya Zaidi, pale ambapo dalili kama kutokwa na majimaji au maumivu wakati wa tendo la ndoa. Seli za kansa ya shingo ya kizazi  hukua taratibu na huchukua miaka michache kwa seli za kawaida kubadilika kuwa seli za kansa, ndio maana inashauriwa kufanya vipimo mara kwa mara ili kugundua mapema.

VISABABISHI VINAVYOPELEKEA KUPATA  SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI.

Wanawake wengi wanaopata ugonjwa huu huwa na kisababishi kimoja au zaidi kinachojulikana ambacho huongeza hatari ya kuupata. Vifuatavyo ni visababishi vikuu:

 1. Kuanza vitendo vya ngono katika umri mdogo (chini ya miaka 16)
 2. Kuwa na mahusiano ya kimwili na zaidi ya mwanaume mmoja
 3. Maambukizo ya virusi vya HPV (Human papilloma virus)
 4. Maambukizo ya magonjwa ya zinaa
 5. Umri zaidi ya miaka 30
 6. Upungufu wa kinga mwilini (VVU/UKIMWI)
 7. Uvutaji wa sigara
 8. Kupata mimba katika umri mdogo
 9. Idadi kubwa ya watoto na kuzaa mara kwa mara
 10. Hali duni ya kiuchumi
 11. Kuwa na mahusiano ya kimwili na mwanaume ambaye mkewe alikufa kwa saratani ya shingo ya kizazi
 12. Kuwa na mahusiano ya kimwili na mwanaume ambaye hajatahiriwa
 13. Historia ya saratani ya shingo ya kizazi katika familia

Kuanza vitendo vya ngono katika umri mdogo na kuwa na mahusiano ya kimwili na zaidi ya mwanaume mmoja ni visababishi vinavyoongoza. Pia maambukizo ya virusi vya HPV (Human papilloma virus), huchangia kwa kiasi kikubwa katika kusababisha ugonjwa huu.

DALILI ZA KUWA NA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI.

Katika hatua za awali za ugonjwa huu kunaweza kusiwe na dalili zozote. Lakini, kadri muda unavyosonga dalili bayana za awali hujitokeza kama:

 1. Kutokwa na damu ukeni kusiko kawaida mfululizo
 2. Kutokwa na damu ukeni baada ya tendo la ndoa
 3. Kupata maumivu makali ya tumbo na nyonga
 4. Maumivu wakati wa tendo la ndoa
 5. Kutokwa na majimaji ukeni kusiko kawaida yenye harufu na maumivu ya tumbo chini ya kitovu.

Muda unavyosonga zaidi, ugonjwa huu unaweza kusambaa kwenda tumboni, mapafuni au popote pale mwilini. Dalili nyinginezo ni kama: maumivu ya mgongo, maumivu ya nyonga, miguu kuuma na/au kuvimba, uchovu, kukosa hamu ya kula, kupungua uzito, kutokwa na damu kwa wingi ukeni, kutokwa na mkojo au kinyesi ukeni (fistula) na kuvunjika mifupa kwa urahisi.

WATU GANI WAPO KWENYE HATARI KUBWA YA KUPATA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI.

Kuna sababu zilizo ndani ya uwezo wako ambazo unaweza kuzifanyia kazi na kuunguza hatari ya kupata saratani hii, japo pia kuna njia ambazo ni vigumu kuepuka za ziko nje ya uwezo wetu kama vile uwepo wa saratani hii katika historia ya familia yako mfano kama mama ama dada yako aliwahi kupata saratani hii basi unaweza kuwa kwnye hatari kubwa nawe kupata. Makundi mengine ni kama

 • Wanawake kwenye umri kati ya miaka 20-50 wapo kwenye hatari Zaidi
 • Matumizi ya vidonge vya kupanga uzazi kwa mda mrefu.
 • Kuzorota kwa kinga ya mwili husabisha kuongzeka kwa athari ya virusi wa HPV wanaoletekeza kansa ya shingo ya kizazi.
 • Wanaopata ujauzito katika umri mdogo chini ya miaka 17 wapo kwenye hatari Zaidi ya kupata saratani hii.

MATIBABU YA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI.

Tiba ya saratani ya shingo ya kizazi hutegemea na hatua ya ugonjwa husika, na inahusisha

 • Kufanyiwa upasuaji na kuondoa mfuko wa mimba (uterus) na viungo vingine kama ovari na mirija ya uzazi
 • Matibabu kwa kutumia dawa kali(chemotherapy) ili kuongeza muda wa kuishi
 • Matibabu kwa njia ya mionzi ili kuua seli za saratani.
 • Kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu mara kwa mara.
 • Kupata chanjo dhidi ya virusi vya HPV kabla ya kuanza vitendo vya ngono.
 • Kupata elimu sahihi kuhusu ugonjwa huu.
 • Kujiepusha na mambo hatarishi yanayosababisha kuupata ugonjwa huu.
 • Ugunduzi wa mapema katika hatua za awali za ugonjwa huu na kupatiwa matibabu stahiki na kwa wakati.

MAMBO 10 UNAYOWEZA KUFANYA KUPUNGUZA HATARI YA KUUGUA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI

 • Usivute sigara wala kutumia tumbaku ya aina yoyote
 • Hakikisha nyumbani kwako hamna moshi
 • Kula chakula chenye afya
 • Kunyonyesha kunapunguza hatari kwa mama kuugua saratani
 • Hakikisha watoto wako wanapata chanjo dhidi ya hepatatis B na HPV
 • Epuka kuchomwa sana na miale ya jua, au tumia mafuta yanayo kukinga dhidi ya miale hiyo.
 • Punguza uchafuzi wa hewa ndani na nje ya nyumba
 • Jishughulishe kuupa mwili mazoezi
 • Punguza unywaji wa pombe
 • Jitahidi kufanyiwa ukaguzi wa mapema kutambua uwepo wa saratani.

HITIMISHO

Kwa kutegemeana na hatua ya saratani yako ilipofikia Dactari anaweza kukuanzishia aina moja ya matibabu ama ukapata matibabu ya aina Zaidi ya moja, hatua ya mwisho ni kuondoa kizazi kama saratani yako imesambaa sana. Kumbuka hatua hii itasababisha usiwe na uwezo wa kushika mimba tena. Jambo la kuzingatia kwa wewe mwanamke ni kufanya vipimo kila mara walau kila baada ya miezi mitatu ili kujihakikishia usalama wa afya. Pia hakikisha unatumia virutubisho mbalimbali kwa ajili ya kutoa sumu mwilini na kujikinga dhidi ya saratani.