Penny Royal yawavisha viatu wanafunzi Kijini, Mbuyutende

TAASISI ya ‘Best of Zanzibar’ leo imezindua kampeni yake iliyopewa jina la ‘Valisha Mtoto Viatu’ katika skuli za Kijini na Mbuyutende Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja.

Kampeni hiyo imebuniwa baada ya kubainika watoto wa skuli hizo zilizoko kijiji cha Matemwe hutembea muda mrefu mwendo usiopungua kilomita tano kwenda na kurudi skuli kwenye ardhi kavu na yenye mawe bila ya viatu.

Katika hatua ya awali, jumla ya jozi 200 za viatu ziligaiwa kwa wanafunzi wa skuli hizo, lengo ikiwa kugawa jozi 1,500 ndani ya miezi miwili, huku kukiwa na taarifa kwamba wadau na wahisani mbalimbali waliovutiwa wamekuwa wakiahidi kuchangia viatu vya ziada.

Hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya skuli ya Kijini, pia iliambatana na utoaji zawadi za mikoba ya skuli kwa wanafunzi 45 waliofanya vizuri katika program ya mafunzo ya ziada iitwayo ‘After –hours Tutoring Program’ inayowanoa katika masomo ya Kiingereza na Hisabati.

Aidha, mwanafunzi Makame Kidawa Mwiga aliyefaulu michepuo pamoja na Vuai Ali Haji, ambaye ni pekee aliyeingia kidato cha tano mwaka huu, nao pia walizawadiwa kwa kuwa mfano mzuri kwa wenzao.

Akizungumza na wanafunzi wa skuli mbili hizo pamoja na wazazi, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Vuai Mwinyi Mohammed, aliwataka wana wa vijiji hivyo kuthamini juhudi za kuleta mabadiliko zinazochukuliwa na kampuni ya Peny Royal inayofadhili miradi mbalimbali ya kijamii ili kuleta ustawi wa maisha kwao na kwa watoto wao.

Alisema kampuni hiyo inayowekeza mradi mkubwa wa kitalii hapo Matemwe, imepania kwa dhati kuhakikisha inawajengea wananchi wa hapo mazingira mazuri ya kuondokana na maisha duni ikiwemo kuwekeza kwenye elimu.

“Hii ni nyota ya jaha iliyokujieni, hamna budi kuipokea kwa mikono miwili na kuwapa ushirikiano wenzetu hawa wanaotumbukiza fedha nyingi, wakilenga kuviunganisha vijiji vyenu katika mambo ya elimu, kilimo, sanaa, utamaduni na dini yetu. Naomba muwaunge mkono ili wafike tunapotaka,” alisisitiza Mkuu wa Mkoa.

Aidha aliwakumbusha wazazi na walezi wajibu wao wa kuwasimamia vijana wao katika masomo ili wapate elimu nzuri itakayowawezesha kushika kazi zinazotokana na uwekezaji mkubwa unaofanyika kijijini kwao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Elimu ya Maandalizi na Msingi Safia Ali Rijaal, aliwasisitiza wanafunzi wa skuli hizo kuelekeza nadhari zao katika masomo, akisema elimu ndio ufunguo utakaoweza kuwatoa katika dimbwi la umasikini na kustawisha maisha yao na kukiendeleza kijiji chao.

“Zawadi hizi ziwe ni ufunguo kwa wanafunzi wengine kuongeza bidii katika masomo ili mje mkijenge kijiji chenu mtapomaliza elimu ya juu,” alieleza Mkurugenzi huyo.

Aliwataka wazazi kuhakikisha watoto wanasoma badala ya kuendekeza vikundi viovu na michezo isiyokwenda na maadili ya Kizanzibari.

Aidha, aliwaomba  kuwasimamia vyema watoto wao na kuhakikisha wanavaa viatu walivyogaiwa, ambavyo alisema ni muhimu katika kulinda afya zao kwa kujiepusha na vitu vya hatari na uchafu unaoweza kuwasababishia maradhi.

Alitumia nafasi hiyo kuishukuru kampuni ya Penny Royal kupitia ‘Best of Zanzibar’ kwa programu zake mbalimbali ilizobuni ili kukiletea maendeleo kijiji cha Matemwe na wananchi wake.

Naye Meneja wa Penny Royal Saleh Mohammed Said, aliahidi kuwa wataendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali za huduma za jamii zinazowakabili wananchi wa Matemwe na vijiji vinavyowazunguka, kwa lengo la kuking’arisha kijiji hicho ili kiwe mfano wa maeneo mazuri kuishi.

Akitoa shukurani kwa niaba ya wana Matemwe, Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Ali Makame Khamis, aliwatanabahisha wazee wa kijiji hicho kutowaacha mkono watoto wao kwa kuwaamini watu wasiokuwa na nia njema na Zanzibar.

“Ni wajibu wetu kuwashika watoto hawa ili wasikilize na kutii maelekezo yetu kwa kusoma kwa bidii badala ya kuwaachia waburuzwe na watu wanaotaka kuwapoteza. Sisi tumekwisha na tunaondoka, tusipojikaza watoto hawa watakuja kuwa bomu ambalo likiripuka litaleta majanga kwa nchi,” alieleza.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Hassan Ali Kombo, Ofisa Elimu Wilaya hiyo Mshamara Chum na maofisa wengine wa Chama cha Mapinduzi na serikali.

 

 

MAELEZO-Aprili 11, 2018