Video: Familia ya Lowassa yatoa kauli tuhuma za kutelekeza mtoto

Kufuatia wito uliotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akitaka wanawake wote waliotelekezwa kufika ofisini kwake, Familia ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Lowassa imeibuka na kudai imeshangazwa na mwanamke aliyekwenda Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kudai kuwa ni mtoto wa kiongozi huyo ambaye ametelekezwa.

Mwanamke huyo aliyejitambulisha kwa jina la Fatuma Lowassa alifika ofini hapo na kusema kwamba yeye ni mtoto wa Lowassa na amekuwa akimtafuta baba yake huyo tangu akiwa darasa la sita.

Aliendelea kueleza kuwa, kwa muda wote huo amekuwa akifuatilia bila mafanikio yoyote ndio sababu ameamua kwenda kwa RC Makonda akiamini kwamba atapata msaada na kwamba yupo tayari kupimwa vinasaba (DNA) ili kuthibitisha kuwa yeye ni mtoto wa Lowassa.

Tazama Video: ikimuonesha mwanamke aliyejitambulisha kuwa ni mtoto wa Lowassa aliyetelekezwa.

Baada ya kusambaa kwa taarifa hiyo, Fred Lowassa ambaye ni mtoto mkubwa wa Mzee Lowassa ameibuka na kueleza kuwa wameshangazwa na kitendo kilichofanywa na mwanamke huyo.

 

Fred alisema kwao mtoto ni baraka na kwamba anashangaa mwanamke huyo kwenda kujitambulisha na kuchafua ukoo mzima kwani kwa desturi zao, huwa hawakatai watoto. Aidha, amekosoa utaratibu unaotumiwa na RC Makonda na kumtaka kukumbuka mbali walipotoka kisiasa.

“Nimesikia mwanamama mmoja akiongea kuwa yeye ni ndugu yetu kule Dar es Salaam..Kwa taarifa tu sisi watu wa Monduli kwetu watoto ni baraka na neema, nimeshangaa ametukosa ukoo mzima kujitambulisha.. Namwambia Paul Makonda, nimetoka naye mbali sana, nasikitika sana anavyotumia nafasi yake vibaya kwa manufaa anayoyajua. Makonda nimekulea.” aliandika Fred.