Hali ya kiungo mshambuliaji wa Prisons na Zanzibar Heroes, Kassim Khamiss bado ni tete

Klabu ya Tanzania Prisons ya Mbeya inayoshiriki ligi kuu soka Tanzania Bara itaendelea kukosa huduma ya kiungo mshambuliaji wake Kassim Suleiman Khamis ambae anaendelea na matibabu ya goti.

Khamis aliiumia goti Disemba 7, 2017 akiitumikia timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) kwenye Mashindano ya Cecafa Senior Chalenj Cup ambapo Heroes waliwafunga ndugu zao Tanzania Bara kwa mabao 2-1, mabao ambayo amefunga yeye mwenyewe Khamis pamoja na Ibrahim Hamad Hilika, mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Kenyatta Machakos nchini Kenya.

Katika mchezo huo uliokuwa mkali Khamis aliumia baada ya kugongana na Daniel Lyanga wa Kilimanjaro Stars na kupelekea kukosa Mashindano yote ya Cecafa msimu uliopita pamoja na kutoitumikia klabu yake ya Prisons ya Mbeya.

Akizungumza na Mtandao huu Khamis amesema anaendelea na matibabu na atokosa mechi zote zilizobakia kwa msimu huu huku akitarajia kujifua kwaajili ya kujiandaa na msimu ujao wa mwaka 2018-2019.

“Bado goti linanisumbua na sasa naendelea na dozi nilizopewa na Daktari, mazoezi madogo madogo nishaanza lakini daktari kaniambia nikae miezi 2 kisha nianze mazoezi kwaiyo timu yangu ntaikosa msimu wote huu, wakati mwengine najisikia unyonge natamani niwepo na wenzangu nicheze lakini Mungu amepipangia hivi na ndio kheir yangu mana huwezi kujuwa mbele yangu kuna nini”. Alisema Khamis.

Katika mashindano ya Cecafa Senior Chalenj Cup yaliyofanyika mwaka jana nchini Kenya ambapo Zanzibar Heroes walishika nafasi ya pili baada ya kufungwa na wenyeji Kenya kwa penalty 3-2 kufuatia dakika 120 kumalizana kwa sare ya 2-2 ambapo Kassim ndie aliyekuwa kinara wa kufunga mabao kwa upande wa Zanzibar baada ya kufunga mabao mawili yote akitokea benchi katika michezo Heroes iliposhinda 3-1 dhidi ya Rwanda na ule wa 2-1 dhidi ya Tanzania bara.

Na Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.