Maharusi wafanya mtihani kabla ya kupewa cheti cha ndoa

Wanafunzi Dorcas Atsea na Deborah Atoh wa Chuo kikuu cha Benue kilichopo nchini Nigeria, wamejikuta wakifanya mtihani siku waliyotakiwa kufanya sherehe ya harusi yao.

Wanawake hao waliokuwa wakiolewa na wanaume wawili tofauti, walijikuta katika hali hiyo ngumu baada ya mtihani mmoja wa chuo wanachosomwa kuahirishwa na kutakiwa kufanyika katika siku waliyopanga kufunga harusi zao.

Kutokana na umuhimu wa vyote viwili (mtihani wa chuo na ndoa), wanawake hao walijikuta wakishindwa kuchagua kimojawapo na kuamua kufanya vyote kwa wakati mmoja.

Siku ya mtihani na harusi ilipowadia, wanawake hao walipambwa vizuri na kumeremeta kisha kuvalishwa magauni yao ya karusi kabla ya kuelekea katika chumba cha mtihani kufanya mtihani wao wa Chuo Kikuu.

Picha za wanawake hao wakiwa katika chumba cha mtihani zilisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii na kuzua gumzo kwa watu wengi walioziona.

Baadhi ya watu wamewapongeza wanawake hao kwa kuipa elimu kipaumbele, kwani licha ya kuwa na tukio la muhimu kama harusi, hawakujali na badala yake wakafanya mtihani kwanza ndipo harusi ikafuata hapo baadae.