Tuhuma za kutelekeza mtoto Lowassa asema hayupo tayari kupima DNA

Waziri Mkuu mstaafu ambaye kwa sasa ni mjumbe wa kamati kuu Chadema, Mhe. Edward Lowassa amevunja ukimwa na kuzungumza kwa mara ya kwanza tangu kuzuke tuhuma kuwa ni mmoja ya viongozi wakubwa wa kisiasa nchini waliotelekeza watoto.

Mhe. Lowassa amekanusha tuhuma hizo na kusema kuwa yeye hana mtoto aliyemtelekeza na hamfahamu kabisa msichana huyo, bali anachokiona ni masuala ya kisiasa yanayoendelea kwenye zoezi hilo la kusaidia akina mama waliotelekezwa na waume zao jijini Dar es salaam ambalo linaratibiwa na RC Makonda.

Wewe unamuamini kweli huyo msichana? angekuwa mtoto wangu kweli ningeshamchukua muda mrefu, kwanza wala simjui naona siasa zinaingizwa hapo kwenye zoezi hilo,amesema Mhe. Lowassa kwenye mahojiano yake na gazeti la Nipashe.

Kwa upande mwingine, Mhe. Lowassa amesema kuwa hata kama akitumiwa barua ya wito kwenda kuonana na Mkuu wa Mkoa hata fanya hivyo kwani ni kupoteza muda, pia amekataa katu katu kupima vipimo vya DNA kuthibitisha kama msichana huyo ni mtoto wake.

Kupima DNA huo ni upuuzi, yaani nipoteze muda wangu kwenda kufanya ujinga huo? sipo tayari,amesema Mhe. Lowassa.

Jumatatu ya Aprili 09, 2018 Msichana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Fatma alijitokeza kwenye ofisi za mkuu wa mkoa wa Dar es salaam kwenye zoezi la kusaidia akina mama waliotelekezwa na waume zao na kudai kuwa Mzee Lowassa ni baba yake mzazi.

Hata hivyo, Mama mzazi wa mtoto huyo akiongea na Bongo5 amesema kuwa ameshawahi kuhangaika kipindi cha nyuma kumtafuta lakini jitihada ziligonga mwamba.