CUF yaomba kukutana na Dkt. Shein

Mjumbe wa Baraza la wadhamini wa chama cha wananchi( CUF) Mussa Haji Kombo amewaomba viongozi wa chama hicho kukutana naRais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi dkt. Ali Mohamned Shein kwa ajili ya kumaliza mgogoro wa kisiasa ambao umechangiwa na CUF kususia katika uchaguzi mkuu wa marudio mwaka 2016.Kombo alisema hayo wakati alipokutana na waandishi wa habari hapo katika hoteli ya Sea cliff iliopo Malindi na kuelezea hali ya kisiasa ya Zanzibar pamoja na mgogoro uliopo ndani ya chama hicho kati ya mwenyekiti wa chama hicho Professa Ibrahim Lipumba pamoja na katibu mkuu wa chama hicho Seif Sharif Hamad.

Aliyo ya sema Vanessa mdee baada ya Jux kusaini dili nchini China

Alisema mgogoro wa kisiasa uliopo sasa ambao umechangiwa na chama cha CUF kushindwa kumtambuwa Rais wa Zanzibar aliyeshinda kihalali katika uchaguzi wa marudio wa Machi 2016 hauna tija na kwa kiasi kikubwa upo kwa ajili ya kuzorotesha demokrasia na kujenga mazingira ya chuki na uhasama.

Alifahamisha kwamba chama cha CUF kilifanya makosa makubwa kususia uchaguzi huo,ambapo matokeo yake ni kukosa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika majimbo 18 ya kisiwa cha Pemba ambayo kwa kawaida hushikiliwa na chama hicho chenye idadi kubwa ya wafuasi.

”Njia pekee ya kumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar na kujenga siasa za kiungwana na kistaarabu viongozi wa chama cha CUF wanapaswa kukutana na rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi dkt Ali Mohamed Shein kwa ajili ya kujenga Zanzibar yenye mshikamano na upendo”alisema.

Alisema Wazanzibari wanahitaji umoja na mshikamano na sio chuki na uhasama kwa kugawanywa katika majimbo na mikoa ikiwa ni moja ya hatua ya kuelekea katika serikali ya umoja wa kitaifa itakayowaunganisha wananchi wote kwa ajili ya kuleta maendeleo.

Akizungumzia mgogoro unaokikabili chama cha wananchi CUF kiasi ya kuwepo kambi ya Lipumba pamoja na Maalim Seif,alisema malumbano yanayokikabili chama hicho hayana tija ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakidhoofisha chama na kujenga siasa za chuki na uhasama kwa wanachama na wafuasi wake kwa ujumla.

Alisema Maalim Seif kwa sasa amepoteza muelekeo wa kisiasa na dira ya kuongoza chama hicho huku akijenga chuki na uhasama kwa viongozi wa chama kwa wale anaowatilia mashaka wenye nia ya kugombea nafasi mbali mbali ikiwemo yake ya ukatibu mkuu au kuwania nafasi ya urais.

Kwa mfano alisema hivi karibuni amewafukuza viongozi wengi wa chama hicho waandamizi na waasisi kwa hofu tu ya kutofautiana naye na wasiwasi wa kuchukuwa nafasi yake ya katibu mkuu pamoja na kuwania nafasi ya urais katika chama hiccho,ambapo yeye amekuwa mgombea wa kudumu tangu mwaka 1995 tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

”Katibu mkuu wa chama cha wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad kwa sasa amepoteza muelekeo wa kukiongoza chama ambapo ni bora kukaa pembeni kwa sababu amekuwa akijenga hofu na chuki kwa viongozi waandamizi wa chama hicho kwa wale anaotofautiana nao kimtizamo na muelekeo wa kisiasa”alisema.

Chama cha wananchi CUF kimekumbwa na mgogoro mkubwa wa uongozi ambapo mwenyekiti wa chama hicho taifa Professa Ibrahim Lipumba ametangaza kumfukuza kazi Katibu mkuu wa chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad,ambaye na yeye ametangaza kumfukuza nafasi ya uenyekiti Professa Lipumba.