Kitendo cha vyama vya siasa kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara kutaathiri

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Cecilia Pareso amesema kitendo cha vyama vya siasa kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara kutaathiri juhudi za wanawake kushiriki sawa na wanaume katika nyadhifa mbalimbali.

Akizungumza katika mahojiano, Pareso alisema: “Natamani wanawake wengi kushika nyadhifa mbalimbali na hilo lingewezekana kama mikutano ingekuwapo ya kuwahamasisha.

“Serikali imekataza mikutano ya hadhara kinyume cha sheria na Katiba… shughuli za vyama zimeainishwa katika sheria (ya vyama vya siasa) ya mwaka 1992 moja ya kazi hizo ni mikutano ya hadhara.”

Pareso alisema chama cha siasa ni wanachama na ili vyama viwepo vinahitaji wanachama.

“Kutofanya mikutano inaweza kuwafanya wanawake hususan wa vijijini kutofikia ushiriki wa asilimia 50 kwa 50 na wanaume,” alisema.

Kuhusu wabunge wa upinzani kukamatwa mara kwa mara, mbunge huyo alisema hatua ya kuwaita polisi na kufikishwa mahakamani kunawaondoa katika hoja ya kuisimamia vyema Serikali.

Pareso alisema kazi ya wabunge ni kupaza sauti kuitaka Serikali ifanye mambo kwa kufuata miongozo, sheria na kanuni na kwamba wanapominywa kutekeleza hayo wanaitwa kuwa si wazalendo.

Alipoulizwa kama kuna siku atahamia CCM, Pareso alisema: “Hapana, si rahisi, nashukuru sana Chadema kwa kunipa nafasi hii, nilianza siasa nikiwa kidato cha sita, nikawa diwani kisha mbunge katika Bunge la kumi na sasa la 11, nakishukuru nitaendelea kutoa utumishi wangu, kukipigania kwani ndicho kimenifikisha hapa.”