Polisi Jamii shehia ya miembe walitolea mbavuni tukio la kuwapiga  vijana katika shehia hiyo

Polisi Jamii shehia ya miembe wamesema hawahusiki na tukio la kuwapiga  vijana wa shehia hiyo na kudai kwamba waliotenda tukio hilo ni jeshi la polisi wakiwa katika doria zao za kawaida.

Hayo yamezungumzwa na  Kamanda Mkuu wa kikosi cha polisi jamii shehia ya miembeni Salum Abdalla Mzee pamoja na Mwenyekiti wa shehia hiyo Yussuf Ali wakati wakizungumza na Zanzibar24 baada ya kutokea kwa malalamiko kuwa  polisi jamii wamewapiga vijana wa maskani ya ccm shehia ya miembeni.

Kwaupande wake kamanda mkuu wa kikosi hicho akitoa ufafanuzi juu ya tukio hilo amesema wao kama polisi jamii wanafanyakazi kwa kushirikiana na wananchi wa shehia hiyo na wala hawadhani kama tukio kama hilo litaweza kutokea katika eneo hilo kwani polisi jamii hawana mamlaka ya kuchukua sheria mikononi mwao.

Wamesema  polisi jamii wanafanya kazi ya kulinda mali na raia katika shehia hiyo pamoja na kuwadhibiti wahalifu wanaofanya hujuma hivyo wamewataka wananchi kuona umuhimu wa uwepo wa kikosi hicho kinachojitolea kwa ajili ya kuweka usalama wa raia.

Aidha Mwenyekiti wa kikosi hicho Yussuf Ali amesema  kazi ya kulinda mali na raia ni kubwa inayohitaji moyo kwani nyakati zinazotumika katika kufanya ulinzi ni usiku hivyo wamewataka wananchi kuwacha tabia ya kuichafua polisi jamii na badala yake watoe mashirikiano ili kufanikisha kazi yao.

Kwaupande wake Sheha wa shehia hiyo ya Miembeni Haji Shomari Haji amekiri kutoa kwa tukio la kupigwa vijana wa shehia lililofanywa na Jeshi la polisi waliokuwa katika kazi zao za doria za usiku za kuwakamata wanaojishirikisha na vitendo viovu.

Haji amesema tukio hilo kwa kupigwa vijana  halihusiani na Polisi jamii kwani polisi hao shirikishi hawajapewa mamlaka ya kuchukua sheria mikononi badala yake wao wakamate wanaofanya vitendo viovu katika shehia na kuwafikisha katika kituo cha polisi kwa hatua zaid za kisheria.

Amina Omar