Mlemavu wa akili azalishwa watoto wawili kwa njia za udhalilishwaji

MAMA mwenye mtoto ambae ana ulemavu wa akili mkaazi wa shehia ya Shengejuu Wilaya ya Wete, amesema  kudhalilishwa kwa mwanawe na kupewa ujauzito ni mitihani kutoka kwa Allah na kamwe hatokwenda kushitaki popote.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi nyumbani kwa mama huyo, alisema kuwa mwanawe huyo ana watoto wawili ambao amewapata kwa njia ya kudhalilishwa, ingawa hajavifikia vyombo vya sheria kuripoti.

Alisema   anaona bora kumshitakia Mola wake kwa kitendo anachofanyiwa mwanawe, kutokana na kuwa anapoulizwa hawatambui wanaomfanyia ukatili huo, hivyo ni vigumu kwenda kuripoti kwenye vyombo husika.

“Kwa kweli ni mitihani kwa sababu kila siku ukimuuliza alikuwa anataja mtu mwengine, kwa hiyo hatujui tumkamate nani, hivyo tumeamua kukaa tu na kumuachia Mungu”, alisema mama huyo.

Mama huyo, aliiomba Serikali kuwasaidia huduma zote ikiwemo chakula, matibabu na malazi ili kuendesha maisha yao, kwani hali yao ni masikini huku watu wakiwaongezea mzigo katika familia.

“Nashindwa hata kuwahudumia watoto vizuri huduma zinazostahiki, kwani mwanangu ni mlemavu wa akili na sasa ana watoto wawili wanaohitaji kushughulikiwa”, alisema mama huyo.

Nae dada wa msichana huyo, alisema kuwa  hali  ya watoto hao hairidhishi kiafya kutokana kukosa chakula chenye lishe bora na kwa wakati, hali ambayo inapelekea kudhoofika kimwili pamoja na kuvamiwa na maradhi ya kila aina.

“Kwa kweli ni mitihani lakini anavyofanyiwa mdogo wangu ni ukatili mkubwa, familia yetu ni masikini na bado watu wanatuongezea mzigo”, alisema dada huyo.

Nae msichana huyo mwenye ulemavu wa akili, alisema kuwa  aliyembaka na kumpa ujauzito mara ya pili anamjua ni mkaazi wa Mgogoni Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini, ambae alikwenda shengejuu kutembea kwa jamaa zao na ndipo aliposubiri wazazi wake wamekwenda shamba na kwenda kumbaka nyumbani kwao.

“Alikuja nyumbani watu hawapo akanibaka, nilipokuwa na mimba nilimwambia lakini alikimbia na kwenda Mgogoni hadi leo sijamuona na wala haniletei huduma”, alisema.

“Mwanangu hapati chakula mpaka watu warudi shamba wapike, tunakula usiku, maana sina pesa ya kumnunulia chakula chakumpikia, hivyo hukaa na njaa muda mrefu na maziwa hayamshibishi tena”, alisema.

Msaidizi mratibu wa shehia hiyo, Maryam Said Ali, alisema   wakati wa tukio hilo kutokea walikwenda kuwashauri wazazi wafike vyombo vya sheria kuripoti, ingawa walishindwa kwa madai kuwa hamtaji mmoja anapoulizwa mtoto wao.

“Mara zote tulizokwenda alikuwa anamtaja huyo huyo, kinachonishangaza wazazi wanasema eti anataja wengi hawajui wakamate wapi, lakini ninavyoona wanakataa muhali maana huyo mwanamme ni katika familia yao na ndio maana hawakufika kwenye vyombo vya sheria kuripoti”, alisema Mratibu.

Nae ,Sheha wa shehia hiyo, Omar Faki Kombo, alisema kuwa wazazi wa msichana huyo wamekuwa hawasemi mara zote anazowafuata kutaka taarifa, jambo ambalo limepelekea kesi hiyo kutoshughulikiwa.

“Wazazi hawako tayari kusema hili, pia mtoto mwenyewe hana mtu mmoja anaemtaja nimelibaini hilo, hivyo tunaomba vyombo vya sheria pamoja na wadau mbali mbali kushirikiana kwa pamoja, ili kuona msichana huyu anapata haki zake za msingi na huduma”, alisema sheha huyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Haji Khamis Haji, alisema   hajapokea taarifa hiyo na kuwataka wananchi wasivunjike moyo katika kuripoti kesi hilo, ili kuweza kupata haki zao za msingi.