Zanzibar yaadhimisha siku ya Wakunga Duniani

Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohammed amewataka Wafanyakazi wa Wizara ya afya kuwa na utamaduni wa kufanya tafiti zinazohusiana na taaluma yao ili kujijengea uwezo wa kutoa huduma bora kwa wagonjwa.

Akizungumza katika Maadhimisho ya siku ya Wakunga yaliyofanyika katika Ukumbi wa Baraza la wawakilishi la zamani Mjini Zanzibar, Waziri Hamadi amesema Wafanyakazi wa Afya watakapojikita katika kufanya tafiti zitaweza kuwasaidia wagonjwa  kunufaika na huduma za matibabu kwa haraka.

Amesema nchi zinakuwa kimaendeleo kutokana na Wafanyakazi wao kuwa na utamaduni wa kufanya tafiti mbalimbali jambo ambalo linarahisisha upatikanaji wa taarifa na mahitaji ya Wananchi ili yaweze kupatiwa Ufumbuzi.

Hata hivyo amelitaka baraza la Wakunga na Wauguzi kuwachukulia hatua za Kisheria Wakunga na wauguzi watakao bainika kufanya kazi kinyume na Maadili yao ikiwemo kutoa lugha chafu kwa wagonjwa ili kulinda heshma ya kazi hiyo.

Amesema kuna baadhi yao wanafanya kazi kinyume na maadili na kusababisha wagonjwa  kukosa haki zao za msingi wakati wanapohitaji matibabu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wakunga Valeria Rashid Haroub amesema,  Takwimu zinaonesha Wanawake wapatao 95 kati ya Wanawake Elfu moja Zanzibar wanafariki kutokana na matatizo mbalimbali wakati wa kujifungua.

Amesema tatizo hilo linatokana na baadhi ya kina mama kutofuata elimu ya afya juu ya kwenda kujifungulia katika Vituo vya afya ambavyo wataweza kupata matibabu ya haraka wanapokutana na tatizo wakati wa kujifungua.

Amesema katika kupunguza tatizo la Vifo vya kina mama na watoto wakati wa kujifungua ni vyema kwa Wizara ya afya Kuengeza wataalamu  na vifaa katika Vituo vilivyo karibu na jamii ili kuwawezesha  wazazi kwenda kujifungulia vituoni  na kuachana na tabia ya kujifungulia majumbani .

Kwa upande wake Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa UNFPA Batula Abdi Hassan amesema Shirika hilo wataendelea kushirikiana na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha wanaokoa Vifo vya kina mama na watoto.

Amesema ili lengo la kupunguza vifo vya kina mama na watoto liweze kufikiwa ni vyema kwa wizara ya afya kuangalia namna ya kuongeza wafanya kazi wa wizara hiyo hususani wauguzi na wakunga ili kuokoa vifo vya kina mama na watoto.

Aidha amesema  takwimu zinaonesha Zanzibar ina Idadi ndogo ya wafanyakazi katika Wizara hiyo ambapo watu Elfu kumi wanahudumiwa na wafanyakazi tisa wakati kitaalamu watu elfu kumi wahudumiwe na Wahudumu 23.

Siku ya Wakunga Duniani huadhimishwa kila ifikapo Mei 5 ya kila mwaka ambapo Zanzibar siku hiyo imeadhimishwa katika ukumbi wa Baraza la wawakilishi la zamani ikiwa na ujumbe usemao WAKUNGA NI VIONGOZI KATIKA KUTOA HUDUMA BORA.

Baadhi ya Wauguzi wa Zanzibar walioshirki maadhimisho ya siku ya Wakunga Duniani wakiwa katika maandamano kuelekea Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni ambako maadhimisho hayo yalifanyika rasmi ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed.

 

Mwenyekiti wa Baraza la Wauguzi na Wakunga Zanzibar Bi. Amina Abdulkadir Ali akzungumza na wakunga katika maadhisho hayo yaliyofanyika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Mwakilishi kutoka Shirika la Kimataifa linaloshughulika Idadi ya watu (UNFPA) Batula Abdi Hassan akizungumza na wauguzi walioshiriki maadhimisho ya siku ya wakunga Duniani katika Ukumbi wa Baraza la Wawawkilishi la zamani Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akimkabidhi cheti mmoja wa Wauguzi bora Bi. Rose Abdalla ambae ni mkufunzi mwandamizi kutoka Chuo cha Taaluma ya Sayansi za Afya ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashind Mohamed akizungumza na wakunga katika maadhimisho ya siku ya Wakunga Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Wawawkilishi la zamani Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Wauguzi kutoka vituo mbali mbali vya Afya Zanzibar walioshiriki maadhimisho ya siku ya Wauguzi duniani wakimsikiliza Waziri wa Afya (hayupo pichani) katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni (PICHA NA ABDALLA OMAR – MAELEZO ZANZIBAR).
Wauguzi kutoka vituo mbali mbali vya Afya Zanzibar walioshiriki maadhimisho ya siku ya Wauguzi duniani wakimsikiliza Waziri wa Afya (hayupo pichani) katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni (PICHA NA ABDALLA OMAR – MAELEZO ZANZIBAR).

Na: Fat-hiya Shehe Zanzibar24.