Balozi Seif awataka makatibu kuwa wasiri ili kuhifadhi faragha za Serikali

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif Ali Iddi alisema Makatibu Mahsusi Nchini wanapaswa kuelewa kwamba wanawajibika na jukumu zito na la lazima katika kuendelea kuwa wasiri ili kuhifadhi faragha za Serikali pamoja na Wakuu wao wa Kazi.

Alisema nafasi ya Makatibu Mahsusi wa Taasisi za Umma na hata zile Binafsi wana uelewa mpana unaowapa nafasi ya kujua mambo na siri nyingi za Kiofisi wanazolazimika kuziengaenga muda wote wa majukumu yao ya Utumishi.

Akiufungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania {TAPSEA} unaofanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu Cha Taifa Zanzibar {SUZA- HALL} Tunguu Balozi Seif Ali Iddi alisema uvujishaji wa siri za Ofisi ni kinyume cha Maadili ya Utumishi wa Umma na Misingi ya Kada ya Ukatibu Muhtasi.

“ Ni muhimu kutunza siri. Kwa nafasi zenu mnayajua mengi ya Kiofisi na ya Kibinafsi, hivyo katika kazi zenu ni lazima muwe wasiri ili kuhifadhi faragha za Serikali na za Wakuu wenu wa Kazi”. Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema madhara ya kitendo cha kutoa siri yanakuwa makubwa kiasi kwamba wageni na Wananchi wanaohitaji huduma za Ofisi zao wanapata Taswira mbaya ya utendaji wao wakati Taasisi na Wakuu wao wa Kazi wanategemea uhodari na bidii zao za uwajibikaji.

Aliwashukuru na kuwapongeza Makatibu Muhtasi Nchini kwa usaidizi wao uliowawezesha Viongozi Wengi Serikalini katika kipindi cha Miaka mingi iliyopita na hadi sasa kufanikisha utekelezaji wa  majukumu yao kwa ufanisi kupitia msaada mkubwa wa Makatibu Muhtasi hao.

“ Miaka mingi ambayo nimekuwa Mtumishi Serikalini, hasa katika ngazi ya Uongozi, nimefanikiwa kutekeleza majukumu yangu kwa ufanisi kwa kupata msaada mkubwa wa Makatibu Mahsusi ambao nimebahatika kufanya kazi wakiwa wasaidizi wangu wa karibu”. Alisema Balozi Seif.

Hata hivyo alisema majukumu ya Makatibu Muhtasi sio mepesi kama baadhi ya Watu wanavyofikiria kwani bila ya wao Ofisi haziendi hata  kazi hazifanyiki ipasavyo ikizingatiwa wakati wa sasa ambapo Wananchi, na hata Watumishi wenzao wanao uelewa mkubwa wa kutambua stahiki zao katika kupata huduma kwa misingi ya uadilifu, usawa na haki.

Balozi Seif alieleza wazi kuwa kadri ya Makatibu Muhtasi hao  wanavyoonyesha uchangamfu na ukarimu kwa wageni, Wananchi na hata Wateja wao, ndivyo wapatiwa huduma hao wanavyoondoka na taswira nzuri  kwao, Wakuu wao wa kazi pamoja na Taasisi zao kwa jumla.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi  Seif  aliwahimiza Makatibu Muhtasi wote Nchini kujiendeleza kitaaluma kupitia fursa mbali mbali zinazopatikana hapa Nchini na baadhi ya zile zinazotolewa nje ya Nchini.

Balozi Seif aliwaeleza wanachama hao wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania kwamba wapo wenzao waliojiendeleza na kufikia ngazi za Watendaji na baadhi yao kufikia kiwango cha Viongozi Wakuu katika Serikali na hata Sekta Binafsi.

Alieleza kwamba majukumu ya Makatibu Mahsusi  sio kupiga chapa pekee, hususan katika zama hizi za mabadiliko makubwa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na Utandawazi ndani na Nje ya Nchi.

Balozi Seif alifahamisha kuwa katika zama hizi  za utandawazi kila Kiongozi anajua kupiga chapa, hivyo ni sahihi kuwa Taaluma hiyo kwa Dunia ya sasa imeenda mbali zaidi kwa kutanua mapana yake.

Aliviomba Vyuo vya Utumishi wa Umma Tanzania Bara na Zanzibar  viendelee kuboresha mafunzo na kuwapa Wakufunzi wenye uzoefu wa kutosha katika kufundisha masomo ya Uhazili.

Alifahamisha kuwa hilo ni vyema likaenda sambamba na baadhi ya vyuo vyenye fursa ya kutoa Elimu ya juu kuangalia uwezekano wa kuanzisha Shahada ya Uzamili ili Makatibu Muhtasi wapate fursa ya kujiendeleza na kuongeza weledi katika Taaluma hiyo.

Akitoa pongezi  Maalumu  kwa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania Bara kwa kuanzisha Shahada katika fani ya Uzamili Balozi Seif akatoa rai kwa Mamlaka zinazohusika kushughulikia changamoto mbali mbali zinazowahusu Makatibu Muhtasi hapa Nchini.

Halkadhalika Balozi Seif  aliwasihi Wanachama wa Chama cha Makatibu Muhtasi kukiimarisha Chama chao pamoja na kukitangaza ili hatimae waweze kuwafikia Makatibu Muhtasi wote shabaha ikiwa kusimamia miiko na maadili ya fani ya Uhazili.

Mapema Mwenyekiti wa Chama cha Makatibu Muhsusi Tanzania { TAPSEA} Bibi Zuhura Maganga Mamboleo alisema Chama hicho kilianzishwa baada ya kubaini kwamba Kada ya Makatibu Muhtasi ambayo ina Watumishi  wengi wanaohitaji kupigania haki zao.

Bibi Zuhura alisema zipo hatua zilizoanza kuchukuliwa na Uongozi wa Chama hicho za kupambana na changamoto zinazowakwaza Watumishi wa Umma wa Kada hiyo ikiwemo Mishahara Duni kwa kukutana na Waajiri wa Sekta mbali mbali Nchini.

Alisema suala la kuendelea kushirikiana na Taasisi za Taaluma limepewa msukumo wa pekee na Chama hicho katika kuona kiwango cha upeo wa Taaluma kwa Wanachama hao kinaongezeka kwa lengo la kunyanyua uwezo wa Kitaaluma wa Makatibu Mahsusi.

Pamoja na mambo mengine Mwenyekiti huyo wa Chama cha Makatibu  Mahsusi Nchini {TAPSEA}wamepanga pamoja na ratiba zao za uwajibikaji katika majukumu yao wameazimia wanachama wake kuchangia Damu Salama itakayosaidia kuokoa uhai, Ustawi na Maisha ya Akinamama na Watoto.

Naye Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Zanzibar Mh. Modeline Cirus Castico akitoa salamu kwenye Mkutano huo alisema unyanyasaji wa Watumishi wa Umma unaowakabili zaidi Wafanyakazi Wanawake unaendelea kukemewa na kupigwa vita na Serikali kuu.

Mh. Castico alisema tabia hiyo mbaya inayoonekana kuzoeleka kwa baadhi ya Viongozi wa Taasisi tofauti Nchini na hata Jumuiya za Kiraia inarejesha nyuma kasi ya uwajibikaji jambo ambalo linatia doa na kupunguza kasi ya uchumi wa Taifa.

Akimkaribisha Mgeni rami kuufungua Mkutano huo wa TAPSEA Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nchini Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ya Tanzania Dr. Dorothy Mwaluko alisema changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma kupitia Kada ya Makatibu Muhsusi hivi sasa zinaendelea kufanyia kazi na Serikali Kuu.

Dr. Dorothy alisema Wizara inayosimamia Utumishi wa Umma  na Utawala Bora imeshaandaa Sera ya Mafunzo kwa Watumishi wake wote wakiwemo Makatibu Mahsusi ambayo Watumishi hao wanapaswa kuielewa vyema.

Alieleza kwamba wakati wakiendelea kuwa na subra na ufuatiliwaji wa changamoto zinazowakabili Dr. Dorothy aliwakumbusha Makatibu Mahsusi hao pamoja na Watumishi wote nchini kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia maadili yanavyowaelekeza.

Mkutano huo Mkuu wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania {TAPSEA} pamoja na mambo mengine Wajumbe wake wamejadili mada mbali zilizowasilishwa na Wataalamu waliobobea ikiwemo Kanuni za Makatibu Mahsusi, Hali ya Uchumi Nchini pamoja na changamoto zinazokikabili  Wanachama wa chama hicho.

 Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

11/5/2018.