Taarifa kuhusu kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi TBC Tido Muhando

Mwanasheria wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Gwakisa Mlawa ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kuwa, Bodi ya Wakurugenzi ya TBC haikufahamu chochote kuhusu mkataba ulioingiwa kati ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Tido Muhando na Channel 2 Group Corporation (BV1) ya Dubai.

Mwanasheria huyo alisema kuwa, Mhando anayekabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya TZS 887.1 milioni, aliingia mkataba huo bila baraka za Bodi ya Zabuni ya TBC.

Gwakisa ambaye ni shahidi wa pili katika kesi hiyo, alitoa ushahidi huo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi. Shahidi alisema hakuwahi kufahamu chochote kuhusu mkataba huo hadi alipopokea taarifa za kesi Juni 2012 kutoka upande wa pili wa mkataba, kwamba TBC imekiuka mkataba wa kuwekeza mitambo ya dijitali.

Katika kesi ya msingi, inadaiwa kuwa Juni 16, 2008 akiwa Dubai (UAE), akiwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Tido Mhando kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kutia saidi mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya runinga kati ya TBC na BV1 , bila kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume na sheria.

Katika shtaka jingine, Juni 20, 2008 Tido anatuhumiwa kutumia vibaya madaraka yake alipotia saini makubaliano  kwa utangazaji wa mfumo wa dijitali kati ya TBC na BV1.

Katika shtaka la tatu, anadaiwa kuwa, kati ya Agosti 11 2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kwa kutia saini mkataba wa makubaliano ya ununuzi, usambazaji, kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BV1 na kuinufaisha BV1.

Shtaka la nne, Tido anadaiwa Novemba 16,2008 akiwa Dubai, United Arab Emirates alitumia vibaya madaraka yake kwa kusini mkataba wa makubaliano (kuongeza wakuu wa mkataba ) kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT broadcast infrastructure) kati ya TBC na BVI na kusababisha BVI kupata manufaa.

Katika shtaka la tano, Tido anadaiwa kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008 katika maeneo hayo ya United Arab Emirates aliisababishia hasara TBC ya Sh 887, 122,219.19.

Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa leo  ambapo Jamhuri inawasilisha ushahidi.

Swahili Times.