Askari Polisi Atekwa Mkoani Singida

Askari wa Jeshi la Polisi aliyetambulika kwa jina la PC Ali, ametekwa kisha akapigwa na kuumizwa vibaya na watu wasiojulikana na baadae kutupwa kwenye vichaka, mkoani Singida.
Taarifa kutoka vyanzo vyake vya habari mkoani Singida zimeeleza kuwa tukio hilo lilitokea Alhamisi ya Mei 10, mwaka huu.
Mmoja wa marafiki wa karibu wa PC Ali, ambaye pia ni askari polisi aliyezungumza na Mtanzania kwa sharti ya jina lake kutotajwa gazetini, alisema kabla ya tukio, PC Ali ambaye ni dereva wa Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Mkalama (OCD), alikuwa ameegesha gari baa ambako alikunywa pombe nyingi mpaka akalala usingizi.
“Ali ni rafiki yangu wa karibu alipolazwa hospitali alisema kuwa baada ya kulewa alikutwa na watu ambao inasemekana ni askari wa usalama, walimpiga picha na kuondoka.
“Baadaye aliamshwa na kupewa taarifa za kupigwa picha, akawatafuta na kuwauliza kwanini wamempiga picha bila ridhaa yake.
“Ali aliniambia kuwa walipatanishwa na mkuu wao lakini baadaye alipigiwa simu usiku huo aende ofisini ndipo akakamatwa na kupigwa sana kwa kutumia waya hadi akapoteza fahamu na baadaye kutupwa vichakani.
“Aliniambia baada ya kupata fahamu alijikongoja hadi Kituo cha Polisi Nduguti ndipo akachukuliwa na kulazwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Singida,” alisema.