Dkt. Shein awataka wana CCM tawi la Fuoni Michenzani kutekeleza dhamira ya Chama chao

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein amewataka wana CCM katika Tawi la Fuoni Michenzani kutekeleza dhamira ya Chama chao katika suala zima la kuimarisha chama, na kusisitiza kuwa ushindi wa CCM katika uchaguzi ujao wa mwaka 2020 hauna mbadala.

 

Dk. Shein aliyasema hayo katika ufunguzi wa Tawi la CCM Fuoni Michenzani, Wilaya ya Dimani Kichama, Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo pia, viongozi mbali mbali wa CCM, akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Balozi Seif Ali Idd alihdhuria.

Dk. Shein ambaye pia, ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alisisitiza haja ya wana CCM wa Tawi hilo kukiimarisha chama chao kwa lengo la kuhakikisha CCM inaendelea kuongoza Dola kwa kushinda chaguzi zote zijazo.

Alieleza kuwa kuwepo kwa Tawi hilo jipya kutakamilisha lengo la kuwasogezea karibu wanaCCM wa Fuoni Michenzani huduma zinazotolewa na Matawi ya CCM na kuondokana na usumbufu wa kufuata huduma hizo katika Tawi la Birikani na Matawi mengineyo.

Pia, Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM aliwaleleza viongozi wa chama hicho katika ngazi mbali mbali kuwa wana jukumu la kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Katiba ya CCM, huku wakizingatia mipango na maelekezo ya Ilani za uchaguzi katika vipindi mbali mbali.

Alieleza kuwa kwa kuwa Tawi hilo ni jipya, aliwashauri kufanya kazi ya ziada ya kulitangaza na kuzitangaza shughuli zao kwa wananchi wa eneo hilo na maeneo ya jirani ili wapate wafahamu kuwepo kwake na shughuli zinazofanyika.

Aidha, aliwasisitiza viongozi wa Tawi hilo kuandaa utaratibu maalum wa kujitambulisha kwa wananchi wa eneo hilo na kuwapa wanaCCM anuani zao na ratiba kamili ya uendeshaji wa shughuli za Tawi, ili kuwasaidia wanaCCM.

Dk. Shein, alipongeza hatua hiyo ya ufunguzi wa Tawi hilo ambao umefanyika baada ya yeye kukamilisha ziara za kuonana na Mabalozi wa Unguja na Pemba, ziara iliyoanza Wilaya ya Mkoani tarehe 2 Mei, 2018 na kumaliza Unguja tarehe 8 Mei 2018 katika Wilaya hiyo ya Dimani Kichama.

Aliongeza kuwa Mikutano hiyo ilifana sana na imedhihirisha uimara wa Chama hicho katika ngazi za Shina na Matawi na imedhihirisha nguvu, umoja na umakini wa Mabalozi katika kuendesha na kusimamia shughuli za Chama katika maeneo na Matawi yao.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, aliwakumbusha WanaCCM hao kuwa jukumu la Chama hicho hasa ngazi ya Tawi ni kukiimarisha Chama, ili kiwe imara zaidi chenye wanachama madhubuti, wanaoongezeka siku hadi siku huku akieleza kuwa hakuna chama kinacholingana na CCM katika kuimarisha Matawi na Mashina yake hata kimoja

Aliwataka wanaCCM wa Tawi hilo kulitumia Tawi lao kwa kufanya kazi za siasa kwa kuendeleza na kukiimarisha chama hicho ili kizidi kupata mafanikio.

Kubwa zaidi lilombelekwa Tawi hilo na Matawi mengine ni kutafuta ushindi wa CCM, na kusisitiza haja ya kuwapitia wanachama katika maeneo yao, kuwakumbusha na kuzungumza na wanachama wa Chama hicho pamoja na wazee, kazi ambayo imefanywa tokea wakati wa ASP.

Dk. Shein alisisitiza kuwa lugha iliyopo hivi sasa kwa wananchama wa Tawi hilo pamoja na Matawi mengine ya CCM ni kutafuta ushindi katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020 huku akisisitiza kuwa CCM si chama cha mtu mmoja bali ni chama cha Wanachama wote na ndio maana kimekwua kikipata mafanikio makubwa.

Alieleza kuwa sifa zote zilizopo hivi sasa kwa Serikali zote mbili ni sifa za CCM kwani ndio chama kiliochopo madarakani.

Aliwasisitiza wanaCCM wa Fuoni Michenzani kulitumia vyema Tawi hilo katika kutafuta ushindi wa uchaguzi wa 2020 kwani kiliopo mbele ya Chama hicho hivi sasa ni ushindi.

Dk. Shein alieleza kuwa hakuna chama kinachoweza kushindana na CCM na kusisitiza kuwa mnamo mwaka 2020 ushindi ndani ya chama hicho ni lazima na kuwataka WanaCCM wa Tawi hilo kuhakikisha Tawi lao linakuwa wazi kwa muda wote ili waweze kufanya shughuli za chama.

Alisisitiza haja ya kulienzi na kulitunza Tawi hilo na kueleza kuwa CCM ni chama kikubwa ambacho kina historia kubwa.

“Kama kuna mtu kafurahi sana basi mie nimefurahi sana.. leo sikukuu…na watu wote wa Fuoni Michenzani wamefurahi”, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwapongeza wale wote waliochangia katika ujenzi wa Tawi hilo.

Aidha, Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, alitoa shukurani kwa wale wote waliochangia katika ujenzi wa Tawi hilo na kuahidi kuwa eneo lote lililombele ya Tawi hilo ambalo lina viwanja atahakikisha utaratibu maalum unafanywa ili limilikiwe na Tawi hilo na wahusika wa viwanja hivyo watapewa viwanja vyengine ili Tawi hilo liwe na nafasi zaidi kama walivyoomba.

Alipongeza wanaCCM wa Tawi hilo kwa kusimamia wenyewe ujenzi na kuepelekea kutumia fedha kidogo zaidi huku akilipongeza Tawi hilo kwa kuwa na Kamati ya Siasa yenye vijana wengi ambao alisema watasaidia kukiimarisha chama chao.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi, alipongeza zilizochukuliwa na Tawi hilo katika kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi huku akiahidi  kutoa Kompyuta na printa kutoka ofisini kwake.

Nae Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi Mohammed Rajab Soud alimpongeza Rais Dk. Shein kwa juhudi zake kubwa alizozichukua katika kuhakikisha Tawi hilo linajengwa kwa msaada wake mkubwa wa ununuzi wa kiwanja hicho.

Katika taarifa ya ujenzi wa Tawi hilo iliyosomwa na Katibu wa Tawi  Ibrahim Abdalla Mwinyi ilieleza kuwa WanaCCM wa Tawi hilo walikuwa na wazo la muda mrefu la kuanzisha Tawi jipya katika eneo hilo baada ya kuona huduma za kichama katika Tawi la CCM Birikani ambalo liko masafa marefu.

Walieleza wazo lakuanzishwa ujenzi wa Tawi hilo liliwasilishwa kwa Dk. Shein kutoka kwa WanaCCM wa eneo hilo wakiongozwa na Marehemu Mzee Ased Ramadhan ambaye yeye ndiye aliyefikisha wazo hilo kwa Makamo Mwenyekiti huko wa CCM Zanzibar.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa mnamo mwaka 2011 alitoa muongozo wa upatikanaji wa kiwanja cha Tawi hilo ambapo wanaCCM wa Tawi hilo walimshukuru na kumpongeza Rais Dk. Shein kwa kuwapa moyo na kuhakikisha wanasimama kidete ili kuhakikisha ujenzi wa Tawi hilo unakamilika.

Walieleza kuwa mwanzoni mwa mwaka 2015 wazo la ujenzi wa Tawi huilo liliibuliwa tena  na vijana wa eneo hilo la Fuoni Michenzani  wakiongozwa na Ibrahim Abdalla Mwinyi ambaye kwa sasa ndie Katibu wa Tawi hilo  na Yahya Lucas Berenga ambaye kwa sasa ndie Katibu Mwenezi wa Tawi hilo.

Aidha, walieleza kuwa mnamo mwaka 2016 Kamati ya ujenzi wa Tawi hilo ulimfuata Mshauri wa Rais Mambo ya Utamaduni Chimbeni Kheir ili awasaidie kutafuta wahisani sambamba na kuchangia hatua zote za ujenzi wa Tawi hilo ambae alikubali na kuifanya kazi yao.

Sambamba na hayo wanaCCM wa Tawi hilo walieleza kuwa ujenzi uliendelea kwa kasi kubwa na nguvu zao kubwa na ndipo ilipofika tarehe 4 ya mwezi Machi mwaka jana 2017 Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Mstaafu Vuai Ali Vuai aliliwekea jiwe la msingi Tawi hilo na mara baada ya shughuli hiyo harambee mbalimbali zilifanyika hadi kufikia hatua hiyo ya kufunguliwa kwa Tawi hilo.

Wanachama hao walitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Shein kwa upendo wake mkubwa aliouonesha kwa kuwa wa kwanza kutoa mchango mkubwa wa upatikanaji wa kiwanja na kuendeleza ujenzi wa Tawi hilo.

Katika ufunguzi wa Tawi hilo burudani mbali mbali zilikuwepo ikiwa ni pamoja na burudani muruwa iliyotolewa na vijana  wa Chipukizi wa UVCCM pamoja na utenzi mwanana uliosomwana Farida Rajab.

Hadi kukamilika kwake Tawi hilo limegharimu TZS Milioni 35.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk