Mambo anayoruhusiwa Lulu kufanya na kutofanya wakati akitumikia kifungo cha nje

Kwa mujibu wa kifungu na 3(2) (a) cha Sheria ya Huduma kwa Jamii ya mwaka 2002 kifungo cha nje ni utaratibu ambao unampa fursa mfungwa kutumikia kifungo chake nje ya gereza kwa kufanya shughuli/kazi zisizo na malipo kwa manufaa ya jamii.

Utaratibu huu hutolewa kwa wafungwa ambao vifungo vyao havizidi miaka mitatu bila kujali wana faini au hawana. Wapo wahalifu wanaohukumiwa moja kwa moja mahakamani kwenda kutumikia kifungo cha nje na wengine huingia gerezani kwanza na baadaye utaratibu wa maombi maalum hufanyika ili mfungwa husika kwenda kutumikia kifungo kwa utaratibu huo.

Baada ya Mwigizaji Elizabeth Michael maarufu Lulu kupewa kifungo cha nje jana, watu wengi wamekuwa wakijiuliza imekuwaje akapewa kifungo hicho, lakini wapo pia waliokuwa wakijiuliza, baada ya kupewa kifungo cha nje, ni mambo gani mengi anaruhusiwa kufanya au harusiwi kufanya?

Mfungwa anayetumikia kifungo cha nje ni lazima aishi kwa kufuata sheria na masharti aliyopangiwa. Masharti hayo ni kuwa chini ya uangalizi maalum, kutoondoka nje ya mkoa bila kibali na kuhakikisha kuwa hatendi kosa lolote mpaka muda wake wa kifungo chake utakapokamilika.

Kifungu cha 4 cha Sheria za Huduma za Jamii kinaipa mahakama nguvu ya kuweka masharti kwa mfungwa atakayekuwa anatumikia kifungo cha nje, ambapo atatakiwa kuhakikisha hakiuki masharti hayo.

Miongoni mwa masharti ambayo mahakama humuwekea mfungwa wa aina hiyo ni pamoja na kwenda kuripoti kwa msimamizi wa huduma za jamii katika eneo husika, kuhakikisha shughuli aliyopangiwa kuifanya anapotumikia kifungo chake nje ya jamii anaifanya kikamilifu, kutoa taarifa kwa msimamizi wa huduma za jamii endapo atabadilisha eneo la makazi na hatakiwi ndani ya muda anaotumikia kifungo cha nje, kutenda kosa jingine.

Masuala mengine kama kusafiri (kutoka nje ya mkoa), kuajiriwa, kuendelea na masomo, au kufanya jambo jingine lolote kunategemeana na masharti yaliyowekwa na mahakama. Endapo mahakama haitakuwa imemzuia mfungwa kusafiri, basi atakuwa huru kusafiri, lakini akiwekewa zuio, hatopaswa kusafiri hadi hapo kifungo chake kitakapomalizika.

Shughuli za kijamii ambazo mfungwa wa nje anaweza kupangiwa kufanya ni pamoja na kufanya usafi katika maeneo mbalimbali mfano shule, hospitali, kwenye fukwe au kushiriki katika shughuli nyingine za kijamii mfano shughuli za mazingira, ujenzi.