SMZ yakiri kuwepo kwa tatizo la ukosefu wa maktaba mashuleni

Serikali ya mapinduzi Zanzibar imekiri kuwepo kwa tatizo la ukosefu wa Maktaba katika baadhi ya skuli za Unguja na Pemba jambo ambalo linarejesha nyuma jitihata za wanafunzi katika kujifunza.

  Akijibu swali katika Mkutano wa kumi wa baraza la tisa la wawakilishi huko Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar, Naibu Waziri Wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali Zanzibar Mmanga Mjengo Mjawiri amesema  licha ya serikali kuendelea kuimarisha sekta ya elimu lakini bado changamoto nyingi zinaikabili ikiwemo suala zima la Maktaba mashuleni.

  Amesema kupitia tathmini iliyofanya kwa skuli za Zanzibar imeonesha katika skuli 129 kwa Unguja asilimia 89 ya skuli hizo hazina maktaba na Skuli 126 za Pemba  asilimia 92 hazina maktaba pamoja na kuwa na idadi ndogo ya Wahutubi .

Amesema takribani skuli zote zinatoa huduma za maktaba katika vyumba visivyo rasmin ambavyo ndani yake vina mchanganyiko wa vitabu ,vifaa vya kufanyia usafi pamoja na Ghala jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.

   Kwa upande wa wahutubi Naibu Mjawiri amesema utafiti unaonesha kuwa ni skuli chache tu ambazo zina wahutubi wenye sifa za kuhutubi na kusema Wizara inaendelea na utaratibu wa kuomba uajiri wa wahudubi waliohitimu katika vyuo hivi karibuni ili kupunguza tatizo hilo.

   Aidha ametoa wito kwa wanafunzi kuwa wavumilivu wakati Serikali inaendelea na jitihada za kuyapatia ufumbuzi matatizo mbali mbali yaliyopo katika skuli za Zanzibar .

Na;Fat-hiya Shehe Zanzibar24.