Balozi Seif awatahadharisha wanachama wanaotishia kurejesha kadi za CCM

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi amewataka wanachama wa CCM hasa Vijana wenye tabia ya kutishia Viongozi kurejesha Kadi za Chama kwa kigezo cha kutaka kutatuliwa haraka changamoto zao kuacha mara moja tabia hiyo ya kuitoa thamani Kadi ya Chama.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Viongozi na Wanachama wa CCM Jimbo la Uzini, Wilaya ya Kati pamoja na Mkoa wa Kusini Unguja mara baada ya kuzindua Rasmi Jengo Jipya la Tawi la CCM Mpapa lililojengwa na Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Moh’d  Raza.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akikata utepe kulizindua rasmi Jengo la Tawi la CCM Mpapa ndani ya Jimbo la Uzini. Nyuma ya Balozi Seif ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mheshimiwa Moh’a Raza Hassanali.

Balozi Seif amewatahadharisha Wananchi hasa Vijana kuepuka kununuliwa Kadi za Chama na Baadhi ya Wanachama wenzao wenye nia ya kugombea nafasi mbali mbali za Uongozi ambapo hatma yake wahusika wa tabia hizo hujenga jeuri na kiuburi na kufikia hatua ya kutoa kauli chafu kwamba fedha zao ndizo zilizowaweka madarakani.

Balozi Seif  alisema Mwanachama yeyote anayekiamini Chama chake kamwe hawezi kufanya kitendo hicho kinachoonesha kutopevuka kimaadili kwa baadhi ya Watu wakati kipindi kilichopita  nyuma Mwanachama huyo aliingia darasani kujifunza Miezi Mitatu kabla ya kupewa Kadi ya Chama.

“ Tunapotaka  kukitia thamani Chama chetu  wanachama Wapya lazima waache tabia ya kununuliwa Kadi jambo ambalo watakuwa wameuza na kununuliwa Utu wao”. Alisema Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa.

Alisisitiza kwamba CCM ni Chama Kikubwa na Kikongwe chenye hadhi na Heshima yake kamili ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Hivyo Wanachama wake wasikubali kuharibiwa Taasisi yao ya Kisiasa na Watu wachache kwa kuendekeza tamaa zao binafsi.