Korea Kaskazini yatishia kufuta mazungumzo kati ya Kim Jong-un na Donald Trump

 

Korea Kaskazini imesema huenda ikaufuta mkutano kati ya kiongozi wake Kim Jong-un na Rais wa Marekani Donald Trump iwapo Marekani itaendelea kusisitiza kwamba taifa hilo la bara Asia ni lazima liharibu au kusalimisha silaha zake za nyuklia.

Mkutano huo ambao umesubiriwa kwa hamu kati ya Bw Trump na Bw Kim unatarajiwa kufanyika mnamo 12 Juni mwaka huu.

 

Shirika la habari la serikali ya Korea Kaskazini KCNA limemnukuu naibu waziri wa mambo ya nje Kim Kye-gwan akisema iwapo Marekani “itatubana na kusisitiza kwamba ni lazima tusalimishe bila masharti silaha zetu za nyuklia basi hatutakuwa tena na hamu ya kushiriki mazungumzo hayo na itatulazimu kutafakari upya iwapo tutakubali mkutano unaotarajiwa kufanyika karibuni kati ya DPRK-US.

Bw Kim amesema Korea Kaskazini “ilikuwa na matumaini makubwa kwamba mkutano huo ungechangia kupunguza wasiwasi katika Rasi ya Korea na kuwa hatua muhimu katika kuunda siku za usoni zenye matumaini makubwa.

“Hata hivyo, inasikitisha sana kwamba Marekani inatuchokoza kabla ya mkutano huo kwa kutoa matamko ya kushangaza.”