Zaidi ya dola million tano za Marekani kutolewa kukarabati jengo la Beit-el-Ajab

Zaidi ya dola million tano za Marekani zinatarajiwa kutolewa na Serikali ya Oman kwa ajili ya matengenezo ya jengo la kihistoria  la Beit-el-Ajab liliopo Forodhani lililojengwa karibu miaka 150 iliyopita.

Hayo yameelezwa  na Waziri wa Habari Utalii  na Mambo ya Kale  Mhe, Mahamoud Thabit Kombo  wakati wa hafla ya kumuaga  Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Kale na Utamaduni wa Oman  Salim Moh’d Almakhrouk baada ya kumaliza ziara ya kutembelea sehemu za historia hapa Zanzibar.

Alisema vifaa kwa ajili ya matengenezo ya jengo hilo utakaosimamiwa na wataalamu kutoka Oman vinatarajiwa kuwasili hivi karibuni na shughuli za ujenzi zitaanza mara tu vitakapo wasili  nchini.

Aidha alisema matengenezo hayo yanatarajiwa kuchukua muda wa miaka miwili na baada ya kumaliza kazi hiyo vifaa vyote  vya ujenzi vitakavyotumika vitaendelea kubakia Zanzibar ili kusaidia ujenzi wa majengo mengine.

 Waziri  Mahmoud Thabit Kombo alisema Serikali ya Oman chini ya Sultani Qaboos  imeonesha nia  kubwa ya kuisaidia  Zanzibar  katika kuimarisha majengo ya mji mkongwe ambao ni moja ya miji iliyomo katika urithi wa kimataifa.

 Aliwashauri wananchi wa Zanzibar kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein za kuwaletea maendeleo  .

 Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Kale na Utamaduni wa Oman  Salim Moh’d  Almakhrouk ameeleza  kuridhishwa  na mashirikiano  mazuri aliyoyapata  wakati wote alipokuwa nchini na ameahidi kuwa Serikali ya Oman itaendelea  kuisaidia  Zanzibar ili kuhakikisha majengo ya kale na yale ya kihistoria yanaenziwa .

 Alifahamisha kuwa baada ya kumaliza matengenezo ya jengo la Beit el Ajab baadhi ya vifaa vya kihistoria vya Zanzibar vilivyopo Oman  vitarejeshwa nchini ili kuzidisha haiba na uhalisia wa awali  na kuongeza vivutio zaidi vya utalii .

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO