Mwanamke aliyehukumiwa kifo kwa kumuua mumewe aliyembaka akata rufaa mahakamani

Msichana raia wa Sudan Noura Hussein ambaye alihukumiwa kifo kwa kumuua mume wake kutokana ya madai kuwa alimbaka amekata rufaa.

“Leo tulikata rufaa kwenye mahakama ya rufaa kupinga uamuzi uliotolewa na mahakama ya chini,” wakili wake Al-Fateh Hussein aliliambia shirika la AFP Alhamsi.

Mahakama ya Sudan ilimpata na hatia Bi Hussein kwa kuua makusudi mapema mwezi Mei baada ya familia ya mumewe kukataa kufidiwa fedha.

Hatma ya Bi Hussein mwenye miaka 19, ilizua maoani kote duniani na hata kuanzisha kampeni iliyopewa jina la #HakikwaNoura

Baba yake Bi Hussein alimlazimisha kuolewa akiwa na miaka 16 na alikua amejaribu kukimbia.

Baada ya ya familia kumkabidhi kwa mume wake, Bi Hussein alisema mume wake aliwaita binamu zake waliomshika huku akimbaka.

Alimdunga kisu na kumua mumewe wakati alijaribu tena kumbaka siku iliyofuati.

Mahakama ya sharia ilimhukumu kifo kwa kunyongwa.

Wakati huo huo kundi la wanaharakati wa kupigania haki za kibinaadamu la Equality Now limesema kuwa litamwandikia rais Omar al-Bashir kumuomba amuonee huruma.

Shirika la Amnesty International limesema kuwa hukumu ya mwanamke ya kifo ambaye alikuwa akijitetea inaangazia uzembe wa serikali kukabiliana na ndoa za watoto , ndoa za lazima na ubakaji katika ndoa.