SMZ yaombwa kutafuta wakandarasi wenye sifa

   Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwapa mikataba ya ujenzi  wakandarasi wenye sifa ili kuepuka  majengo kupata hitilafu kwa muda mfupi.

   Wakichangia  bajeti ya Wizara ya Elimu na mafunzo ya amali zanzibar ya mwaka 2018/19 katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi Chukwani nje kidogo ya mjini wa Zanzibar Wajumbe hao wamesema majengo mengi ya serikali yakiwemo ya skuli yamekuwa yakiharibika wakati yakianzwa kutumiwa.

    Wamesema kitendo hicho cha kuharibika majengo hayo kinatokana na Wakandarasi wanaosimamia kushindwa kufanya kazi zao ipasavyo jambo ambalo linawaletea usumbufu mkubwa wanafunzi hususan katika kipindi cha mvua.

     Amesema pindipo Serikali haitasimamia ipasavyo suala hilo litaweza kuleta athari kubwa  kwa serikali kutokana na kulazimika kutumia fedha za ziada wakati wakihitaji kukarabati majengo hayo.

      Kwa upande wake Mwakilishi wa nafasi za wanawake Saada Ramadhani ameitaka wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali kuwaandalia mazingira mazuri wanafunzi wenye Mahitaji maalumu ili waweze kunufaika na Elimu inayotolewa katika skuli.

     Amesema serikali inahimiza watoto wenye mahitaji maalumu kupelekwa skuli lakini wamekuwa wakikabiliwa na matatizo mbali mbali ikiwemo kukosa nyenzo za kusomea na kukosa walimu wenye sifa za kuwapa elimu inayolingana na wanafunzi wengine.

     Aidha amesema wakati umefika kwa wizara kuangalia namna ya kuajiri walimu wenye sifa za kuwasomesha wanafunzi wenye mahitaji maalumu ili wanafunzi hao waweze kunufaika na elimu inayotolewa na kuweza kuifanyia kazi elimu hiyo baada ya kumaliza masomo yao.

     Akijibu hoja za Wawakilishi hao Waziri wa elimu na Mafunzo ya amali zanzibar Riziki Pembe Juma amesema serikali kupitia wizara ya elimu itahakikisha inayafanyia kazi matatizo yaliyopo ikiwemo la kutafuta mafundi ambao watajenga kwa kuzingatia viwango vya Ujenzi.

     Amesema azma ya serikali ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanapata Elimu sawa na katika mazingira mazuri hivyo watahakikisha wanaimarisha miundombinu ya skuli zote za Unguja na Pemba pamoja na miundombinu ya watu wenye mahitaji maalumu ili waweze kunufaika na elimu iliyopo Nchini.

     Aidha ametoa wito kwa Wajumbe wa Baraza ka Wawakilishi kuunga mkono juhudi za serikali na Wadau wa maendeleo katika kuimarisha sekta ya elimu ili iendane na ulimwengu wa sayansi na teknolojia.