Dr.Khalid: Serikali itaendelea kuwatunza  na kuwathamini wazee

Waziri wa fedha na Mipango zanzibar Dr.Khalid Mohammed amesema Serikali itaendelea kuwatunza  na kuwathamini wazee  wa zanzibar  kutokana  na  mchango mkubwa walitoa katika serikali ya Mapinduzi ya zanzibar.

Akizungumza  na wazee katika hafla ya futari iliyoandaliwa na Mfuko wa hifadhi ya jamii zanzibar ZSSF  amesema wazee  ndio walioijenga nchi ya zanzibar katika  Nyanja zote za maendeleo  kisiasa,kiuchumi na kijamii hivyo serikali haina budi kuthamini jitihada hizo zilizozifanya na wazee hao.

Amesema hatua za ukuwaji wa uchumi  zanzibar umetokana na michango ya wazee  kutokana na  kujitoa na kushirikiana na viongozi katika mapambano ya kutafuta  maendeleo kwa ajili ya taifa  na vizazi vilivyomo.

Hata hivyo Dr Khalid ameupongeza mfuko wa hifadhi ya jamii kwa kuona umuhimu wa kuwajali wazee  kwa kuwafutarisha kwani ni jambo la faraja na lenye heri kubwa ndani yake.

Ametoa wito kwa  watendaji wa mfuko huo kuendelea kuwasaidia wazee si kwa kuwafutarisha tu bali hata kwa kuwasaidia katika mahitaji yao mbalimbali ya kila siku kwani bado wazee wanamahitaji mengi.

Aidha Dokta amewataka wananchi wenye uwezo nao kujitokeza katika kuwasaidia wazee na kutoa msaada kwalengo la kulipa fadhila kwa wazee hao kwani nao walipoteza nguvu zao nyingi katika kulisaidia taifa.

Katika hafla hiyo ya futari iliyoandaliwa na ZSSF ilihudhuriwa na Waziri wa fedha zanzibar ,Waziri wa Kazi,Uwezeshaji,Wazee,Wanawake na Watoto pamoja na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Shadia Suleima Mohammed pamoja na wananchi mbalimbali katika Nyumba za wazee Sebleni.

Amina Omar