Joti kwa mbwembwe, kidogo abebwe na polisi

Msemaji wa Timu Samatta, mchekeshaji Joti aligeuka kituko uwanjani baada ya kuzidisha manjonjo yake kwa kuongeza morali katika timu yake ikishinda mabao 4-2 dhidi ya Timu Alikiba.

Kali zaidi ilikuwa baada ya timu yake kupata penalti, baada ya mchezaji Mbwana samatta kudondoshwa na Agrrey Morris kwenye eneo la hatari ndipo Joti aliingia uwanjani na kumzonga mwamuzi.

Baada ya kuingia uwanjani, mwamuzi alimtoa mpaka nje ya uwanja, lakini bado alionekana kuwa mbishi na kuingia uwanjani, ndipo kocha Jamhuri Kihwelu ‘Julio’, alimfata na kumwambia akae nje.

Polisi waliokuwepo uwanjani walionekana kumfuata na kutaka kumtoa Joti katika benchi, lakini uongozi wa benchi la ufundi la timu Samatta likiongozwa na Julio, walimuomba askari huyo kuachana naye.

Licha ya kusamehewa bado mbwembwe za joti zilizidi kwani alikuwa akiwasindikiza hata wachezaji walipokuwa wanaingia kwenda uwanjani kwa kufanya mabadiliko.

Katika mchezo huo mabao mawili ya mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajib hayakutosha kuisaidia timu Alikiba kuepuka kipigo cha mabao 4-2 kutoka kwa Timu Samatta.

Samatta kwa upande wake alikutana na wakati mgumu ndani ya dakika 30 za kipindi cha kwanza kwa kukabwa vilivyo na Agrey Morris wa Azam na Abdi Banda wa Baroka ya Afrika Kusini.

Kabla ya kipindi hicho cha kwanza, timu Samatta ilitoka nyuma kwa mabao 2-0 na kusawazisha kupitia kwa Mohammed Samatta na mtoto wa Julio, Super kwa njia ya penalti.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku timu Samatta wakionekana kuutawala mchezo na hatimaye kujipatia bao kupitia kwa Haruna Moshi ‘Boban’.

Timu Kiba ilipata kwenye kipindi hicho cha pili, lakini walishindwa kuitumia kwa kufunga bao la kusawazisha kutokana na nahodha wa kikosi hicho, King Kiba kupaisha mkwaju huo wa penalti.