Timu ya Kombaini yajipanga na mashindano ya Rolling Stone

Kocha Msaidizi wa timu ya Kombaini ya Wilaya ya Mjini Ali Bakar Mngazija amesema kuwa maendeleo ya timu yao hiyo yapo vizuri na sasa hivi wamo katika ufundi kutokana na mwezi mtukufu wa Ramadhan hawawezi kufanya mazoezi ya nguvu.

Kombaini ya Wilaya ya Mjini inajiandaa na mashindano ya Rolling Stone ambayo yatafanyika kuanzia Julai 9 mwaka huu, ikiwa ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo kwa mara mbili mfululizo.

Timu hiyo iliyochini ya Kocha Mohammed Seif Kingi imekuwa ikifanya mazoezi yake katika uwanja wa Amaan kila siku asubuhi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika uwanja wa Amaan mara baada ya kumaliza mchezo wao wa kirafiki na timu ya Mwembeladu, alisema kuwa kikosi chao kwa sasa kipo vizuri na wachezaji wamekuwa wakijitahidi na kujituma katika kuonesha uwezo wao.

Alisema kuwa kutokana na jitihada zao hizo za wachezaji ni imani yao kwamba timu hiyo itafanya vyema na kuweza kutetea ubingwa wao.

“Wachezaji wazuri na wanajitahidi kujituma na tunaimani tutatetea ubingwa wetu”, alimalizia kwa kusema.

Na:Ibrahim Makame.