Mtoto wa miaka miwili akutwa ndani ya kisima akiwa ameshafariki Tomondo

Mtoto mwenye umri wa miaka miwili na nusu amekutwa ndani ya kisima akiwa ameshafariki katika maeneo ya wa Tomondo Uzi.

Akithibitisha matukio hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Thobias Sedoyeka, alitaja jina la marehemu kuwa ni mtoto Thulesa Kondo Khamis mkaazi wa Tomondo Uzi.

Alisema mtoto huyo alikutwa ndani ya kisima cha maji na kwa kushirikiana na askari wa zimamoto na uokozi walifanikiwa kuopoa mwili wake na kuufikisha hospitali kuu ya Mnazimmoja kwa uchunguzi na baadae kukabidhiwa jamaa zake kwa mazishi.

Alisema tukio hilo lilitokea Juni 11 mwaka huu saa 4:00 asubuhi Tomondo Uzi wilaya ya magharibi ‘B’ mkoa wa mjini magharibi Unguja.

Aidha alibainisha wanaendelea na upelelezi wa tukio hilo ili kubaini chanzo cha mtoto huyo kukutwa katika kisima hicho.