Muomani anayefanya utalii kwa kwa pikipiki atinga Zanzibar

Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo, amesema ziara inayofanywa na Maher Al Barwani, raia wa Oman kulizunguka bara la Afrika kwa pikipiki ni fursa nzuri ya kutangaza utalii na kupeleka ujumbe wa amani duniani.

Maher (37), yuko Zanzibar takriban wiki moja sasa tangu aingie Afrika, katika mfululizo wa ziara zake alizozianza Julai 22, 2017 kutokea Muscat akipitia Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Saudi Arabia.

Akizungumza ofisini kwake katika hafla ya kumkaribisha Muomani huyo mwenye asili ya Zanzibar, Waziri Kombo amesema kitendo hicho ni cha kishujaa kwani si nchi zote zina amani kama ilivyo Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Alifahamisha kuwa, Zanzibar inajivunia kumuona kijana kama huyo ambaye msingi wa kizazi chake umetokea hapa, kupata wazo la kuitembea dunia kwa njia ya pikipiki yenye manufaa badala ya kukitumia chombo hicho kwa  michezo ya hatari.

Waziri huyo alisema uamuzi wa Maher kufika Zanzibar baada ya kuizunguka Tanzania Bara, ni sahihi kwani ndiko iliko historia ya kuvutia zaidi kuhusu Oman kuliko nchi nyengine yoyote barani Afrika.

Alimtaka awe balozi wa kuitangaza historia ya mafungamano ya Zanzibar na Oman, ambayo watawala wake waliishi na kuacha athari kubwa Unguja na Pemba inayodumu hadi sasa hasa kwenye majengo na vitu vya kale, pamoja na nyaraka mbalimbali.

“Ninakutaka zaidi uitangaze Zanzibar kihistoria, mambo ya kale na amani yake ambayo ndio inayowafanya watalii wanaokuja hapa watembee bila ya khofu na kujihisi wako nyumbani,” alieleza.

Alifahamisha kuwa, uhusiano na udugu wa damu kati ya Oman na Zanzibar ni nakshi iliyochongwa kwenye jiwe ambayo haiwezi kufutika, hivyo uko umuhimu mkubwa wa kuuimarisha kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Akieleza shukurani zake kwa mapokezi mazuri aliyopata tangu alipowasili kisiwani hapa, Maher alisema hakuna tafauti yoyote anayoiona kwani bashasha za Wazanzibari ni kielelezo kizuri kwake kinachomfanya ajielewe kuwa yupo kwao.

Alieleza kufurahishwa kwake na namna alivyofurahiwa katika nchi zote na mikoa ya Tanzania Bara alipokuwa akipita barabarani.

Alisema ziara hiyo si ya kwake binafsi, bali anaifanya kwa lengo la kushajiisha ustawi katika mataifa mbalimbali na amani ili dunia iwe pahala pazuri pa kuishi badala ya kuandamwa na vita na migogoro ya kisiasa.

“Nchi zetu Oman na Zanzibar zimejaa amani na hii ndiyo tunu yetu, tunatamani nchi zote duniani hasa Afrika ziwe mbali na vita ambavyo kwa kiasi kikubwa vinaathiri wanawake na watoto,” alisema baba huyo wa watoto wawili.

Alieleza kuwa, tangu Julai 22, 2017 alipoanza nchini Oman, tayari barani Afrika, ameshafika Sudan, Ethiopia, Kenya, Uganda, Rwanda Burundi na Tanzania Bara kabla hajapanda meli kuja Zanzibar.

Alisema kwa ujumla, tangu alipoanza ziara zake duniani kwa kutumia pikipiki mwaka 2009, ameshatembelea nchi 39 zikiwemo nyingi za Ulaya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Masoko katika Kamisheni ya Utalii Zanzibar Dk. Miraji Ukuti Ussi, alisema wanaichukulia ziara hiyo kama mwanzo wa kushajiisha wapanda pikipiki kubuni mambo yenye tija kwao na kwa nchi yao badala ya kuendesha kwa fujo na kutishia usalama barabarani.

“Baada ya hapa, tutazungumza naye kuangalia uwezekano wa kumfanya awe balozi wetu nchini Oman katika mpango wetu wa kuitangaza Zanzibar ili kulishika soko la utalii katika nchi za ghuba na kwengineko ambako mbawa zetu hazijafika,” alisema.

Hafla ya kumkaribisha, ilihudhuriwa pia na watendaji wakuu wa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale ikiwemo Kamisheni  ya Utalii, pamoja na Balozi mdogo wa Oman hapa Zanzibar, Dk. Ahmed Hamood Al Habsy.

 IMETOLEWA NA WHUMK