Wizara ya Elimu kuendelea kukuza michezo Zanzibar

 

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imesema itaendelea kukuza vipaji vya wanafunzi na kukuza taaluma ili kukuza michezo Zanzibar.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mmanga Mjengo Mjawiri katika ufunguzi wa Tamasha la pili la wazi la mchezo wa Baseball na SoftBall katika viwanja vya Amani majira ya Asubuhi.

Mjawiri amekipongeza chama cha mchezo wa Baseball na Softball Zanzibar (ZABSA) kwa kuendeleza mchezo kwa upande wa Zanzibar ambao unaonekana kama vile bado ni mdogo kwa hapa visiwani Zanzibar.

Katika hotuba yake fupi Naibu Waziri amemtaka mkurugenzi wa michezo wizara ya Elimu kuusambaza mchezo huo kuchezwa kwa kila wilaya ya Zanzibar ili kuwakilisha vizuri kimataifa.

“Sisi wizara ya Elimu tutandelea kuendeleza vipaji kupitia michezo yote na mashindano yetu ya Elimu bila ya malipo nay ale ya Umiseta” alitilia mkazo Naibu waziri wa Elimu.

Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha Baseball na Soft ball Zanzibar (ZABSA) Mwalim Othman Mussa Msabaha amesema mashindano hayo ya pili ya wazi yana lengo la kuutambulisha mchezo huo kwa wananchi kwani bado unachezwa maskulini tu kwa sasa.

Kuhusu mikakati ya chama chao kukuza mchezo huo amesema kila inapofika Disemba huwa kuna mashindano ya Tanzania ili kutafuta timu ya Taifa ya Tanzania ya pamoja  kwa nia ya kuleta umoja baina yao.

“Tumepata nafasi ya kuwa na timu yetu ya Taifa ya mashindano ya Afrika Mashariki kama Zanzibar sisi tutapeleka timu tatu Unguja moja na Pemba moja za wanaume na kwa upande wa wanawake tutafuta mmoja itakayo kwenda Uganda mwezi Disemba tarehe 9 “Alifahamisha Othman.

Aidha amewataka wazanzibari kujitokeza kwa makundi kucheza mchezo huo badala ya kutegemea mpira wa miguu ambao unawachezaji wengi ambao unaweza kukosa nafasi ya kushiriki michuano mikubwa.