Timu ya Madaktari bingwa yatinga Mnazimmoja kutibu ubongo na uti wa mgongo

Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed amewashauri wafanyakazi wa Taasisi ya matibabu ya Ubongo na Uti wa mgongo (NEURO) kujifunza kupitia uzoefu wa wataalamu wa kigeni  wanaokuja Zanzibar ili kuongeza utaalamu.

Waziri Hamad ametoa ushauri huo Hospitali kuu ya Mnazimmoja alipokuwa akiwakaribisha kundi la madaktari bingwa wa NEURO kutoka Marekani, Hispania na Abudhabi ambao watakuwepo nchini kwa ajili ya kambi maalum ya matibabu ya maradhi hayo katika Taasisi Zanzibar.

Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohd akizungumza na Madaktari bingwa wa maradhi ya Ubongo na Uti wa Mgongo kutoka Marekani, Hispania na Abudhabi alipokutana nao katika Taasisi ya NEURO Hospitali kuu ya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.

Alisema madaktari hao wanaotoka Hospitali kubwa katika nchi zao ni wataalamu wazuri na iwapo wafanyakazi wa Taasisi ya Hospitali ya Mnazimmoja watakuwa wabunifu wanaweza kujifunza mambo mengi kutoka kwao.

Waziri wa Afya alisema kambi za mara kwa mara za matibabu ya madaktari bingwa kutoka mataifa mengine ni moja ya fursa kwa madaktari wa Zanzibar kujifunza na kuongeza utaalamu wao.

Aliahidi kuwa Serikali itaendelea na juhudi za kuwasomesha madaktari wa Taasisi NEURO nje ya nchi kila hali itakaporuhusu na kukiimarisha zaidi kwa lengo  la  kupunguza gharama za kupeleka wagonjwa nje kwa ajili ya matibabu.

Alitoa ombi maalum kwa madaktari hao wa kigeni kuwashirikisha na kuwafunza madaktari wa kitengo cha NEURO cha Hospitali kuu ya Mnazimmoja katika operesheni zote watakazofanya.

Aidha amewashauri madaktari hao kufanya utafiti wa kugundua ukubwa wa tatizo la maradhi ya ubongo na uti wa mgongo Zanzibar na kushauri njia zinazoweza kusaidia kupunguza tatizo hilo.

Waziri Hamad amewataka wananchi wenye matatizo ya Uti wa Mgongo na ubongo kutumia fursa ya uwepo wa madaktari hao kwenda kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu bila ya malipo.

Kiongozi wa Madktari hao Prof. Gail Rossean kutoka Chicago Marekani alimueleza Waziri wa Afya kuwa wamefurahishwa na kazi nzuri inayofanywa na Taasisi ya NEURO  ya Zanzibar ya kuwahudumia wananchi na amemuhakikishia wataendelea kuunga mkono juhudi hizo.

Hata hivyo madaktari hao wamesikitika kusikia kuwa hata watoto wadogo Zanzibar wanapata matatizo ya ubongo na uti wa mgongo jambo ambalo sio la kawaida katika nchi wanazotoka.

Hilo ni kundi la nane la Madaktari bingwa wa NEURO kutoka mataifa ya kigeni mwaka huu kuja Zanzibar kwa ajili ya kambi ya matibabu ya maradhi ya Uti wa Mgongo na Ubongo katika Taasisi ya Zanzibar.

Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar