Meli nne saccos watakiwa kuongeza mashirikiano

Waziri Kiongozi Mstaafu ambae ni Mbunge wa Jimbo la Kijitoupele Shamsi Vuai Nahodha amewataka  wanachama wa chama cha ushirika  cha Meli nne saccos kuongeza mashirikiano  kati yao ili kukuza maendeleo  kwalengo la kuinua uchumi kwa wananchi.

Akizungumza  katika Mkutano Mkuu wa tisa wa Meli nne saccos Zanzibar amesema ili kufikia uchumi ambao utainua maendeleo kwa wananchi wa zanzibar lazima wanachama wabadilike na kuwa na mashirikiano ya pamoja  katika vikundi vyao vya  kuweka na kukopa ambapo hatua hiyo itaweza kuleta msukumo wa kufikiwa ile azma ya kumiliki taasisi ya kifedha  kwa ushirika zanzibar.

Amesema  vikundi vya ushirika vimekuwa msaada mkubwa kwa jamii na fedha zinazopatikana  zinasaidia katika miradi mbalimbali ya maendeleo jambo ambalo  huongeza kasi ya ukuwaji wa uchumi na kupunguza umaskini

Hata hivyo Shamsi ametoa wito kwa Viongozi mbalimbali wakiwemo wa Serikalini na wanasiasa  kuekeza nguvu zao katika vikundi vya ushirika na wajasiriamali  ili kusaidia  kuharakisha  upatikanaji wa maendeleo pamoja na kuweza kuifikia ile dhamira ya serikali ya Zanzibar  ya kufikia uchumi wa kati wa viwanda.

Wanachama wa chama cha Ushirika cha Meli nne Saccos wkimsikiliza Waziri kiongozi mstaafu Mh. Shamsi Vuai Nahodha

 

Wanachama wa chama cha Ushirika cha Meli nne Saccos wkimsikiliza Waziri kiongozi mstaafu Mh. Shamsi Vuai Nahodha

Akisoma Risala kwa niaba ya Wanachama wa Meli nne saccos Ramadhan Khamis amesema Meli nne saccos imeweza kupiga hatua nzuri na kufikia malengo  yake waliyojiwekea ya kuinua ustawi wa wanachama na kuondoa hali ngumu ya umaskini na mwanachama kuweza kujitegemea mwenyewe.

Aidha amesema mbali na mafanikio waliyoyapata  hasa katika kuwaelimisha  wananchi kujiunga na vikundi vya ushirika, kutoa elimu kwa wajasiriamali ya uombaji wa mikopo na miradi lakini bado Ushirika unakabiliwa na tatizo la uhaba wa vitendea kazi.

Kwaupande wake Mrajis wa vyama vya Ushirika ambae ni Mkurugenzi  Idara ya ushirika Zanzibar Khamis  Daud Simba  amesema Chama cha ushirika  kina umuhimu mkubwa  hivyo ni vyema kwa wanachama  kukithamini na kuwa na mashirikiano ambayo yatakiimarisha  ili kiweze kudumu.

Simba amewataka viongozi wa Meli nne saccos kuwacha tabia ya  kuwaonea muhali  wanachama waliokuwa  hawafuati  masharti na kanuni za ushirika  badala yake kuwachukulia hatua za kisheria  ili kuondoa matatizo yanayochangia  migogoro kwenye umoja huo wa saccos.

Jumla ya Saccos 221 zipo zanzibar unguja na pemba ikiwemo Meli nne saccos ambazo zimepewa mikopo   ya Shillingi  Billion 19  ambapo  azma ya serikali ya mapinduzi zanzibar  kwa vikundi vya ushirika ni kumiliki  taasisi ya kifedha itayowasaidia katika kuweka na kukopa fedha ambazo zinamasharti nafuu.

Meli nne saccos imeanzishwa  mwaka 2005 ambapo  hivi sasa inawanachama  elfu Moja mia tatu na sabini na tano.

Amina Omar