Mtoto wa miaka miwili afariki kwa kujifyatua risasi kichwani

Mtoto mwenye umri wa miaka miwili amefariki baada ya kujipiga risasi kichwani kwa bunduki ambayo imekuwa ikihifadhiwa na wazazi wake nyumbani kwao.

Bunduki hiyo ambayo hutumia risasi zenye ukubwa wa 9mm ilipatikana eneo la tukio ambayo ilikuwa inamilikiwa na babake.

Kufikia sasa, bado haijabainika iwapo wazazi wake watashtakiwa.

Polisi wa Houston, Texas nchini Marekani wanasema wazazi wa mtoto huyo – Christopher Williams Jr – walikuwa nyumbani wakati wa tukio hilo.

Watoto kadha wamekuwa wakijipiga risasi na kujiua kimakosa nchini Marekani miaka ya karibuni.
Polisi wa Houston wamesema wanajaribu kubaini ni vipi mtoto huyo aliyepewa jina la utani “Junior” aliweza kuifikia bunduki hiyo.

Mkuu wa kitengo cha waathiriwa maalum katika idara ya polisi ya Houston David Angelo ametoa wito kwa wazazi walio na bunduki kuchukua tahadhari zaidi.

“Ni lazima uweke salama silaha, iwe ni kwa kuhakikisha kifaa cha kufyatulia risasi kimewekwa salama au kuiweka salama silaha kwa njia nyingine kuhakikisha matukio kama haya hayatokei tena siku za usoni,” alisema.

Alieleza kisa hicho kuwa cha kusikitisha sana.

Binamu yake marehemu Suzzane Alvarado ameambia ABC 13 kwamba marehemu “hakustahili yaliyomkuta. Alikuwa mtoto mdogo na mwenye matumaini makubwa maishani.”

Kwa mujibu wa gazeti la Houston Chronicle, ambaye ni baba wa marehemu Christopher Charles Williams, alipatikana na hatia ya kuwa na bastola kinyume cha sheria mwaka 2009.