Kiongozi wa DW uso kwa uso na Waziri wa habari Zanzibar

KUONGEZEKA kwa matangazo ya lugha ya Kiswahili katika vituo vingi vya redio duniani, ni fursa nzuri kwa wanahabari wa Zanzibar kupata kazi na ziara za kimafunzo na hivyo kuzidi kuitangaza lugha hiyo.

WAZIRI wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo (Kushoto), akizungumza na Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili Ujerumani (DW) Bibi Andrea Schmidt aliyefika ofisini kwake jana. Kulia ni mtangazaji mstaafu wa Idhaa hiyo Ramadhan Ali ambaye alijiunga nayo akitokea iliyokuwa Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ), na kuitumikia kwa miaka 41

Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale  Mahmoud Thabit Kombo, akizungumza na Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili wa Sauti ya Ujerumani (DW) Bibi Andrea Schmidt aliyefika ofisini kwake leo, amesema hadhi ya Kiswahili imeongezeka na kupata heshima kubwa hasa katika nchi za Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara.

Ameipongeza Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani kwa kuendelea kupokea watangazaji wengi kutoka nchi za Afrika Mashariki, hali aliyosema inatoa chagamoto kwa Wazanzibari kujiendeleza ili kufikia vigezo vinavyotakiwa na Idhaa hiyo na nyengine zinazotangaza kwa lugha ya Kiswahili.

Alisema kimsingi, lugha ya Kiswahili imezaliwa Zanzibar na ndiko nyumbani kwake inakozungumzwa kwa ufasaha na usahihi.

Alieleza kufarajika kwake kwamba vyuo vikuu vingi duniani ikiwemo bara la Ulaya na Mashariki ya mbali, vimeanzisha vitivo vya kufundisha lugha hiyo kwa kiwango cha shahada za juu.

Alieleza haja kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Ujerumani kutanua wigo wa ushirikiano, ili Zanzibar iweze kunufaika na maendeleo ya teknolojia katika tasnia ya habari na mawasiliano.

Waziri Thabit ameeleza kuwa Ujerumani na Zanzibar zina uhusiano wa miaka mingi katika kushirikiana kwenye sekta ya habari, ambapo miaka ya nyuma watangazaji na mafundi kutoka iliyokuwa Sauti ya Tanzania Zanzibar walipata nafasi kufanya kazi kwenye idhaa hiyo pamoja na kubadilishana vipindi.

Ameshauri pande hizo mbili ziangalie uwezekano wa kurejesha utaratibu huo pamoja  na kutafuta maeneo mengine wanayoweza kushirikiana kwenye sekta ya habari inayokua kwa kasi kutokana na mabadiliko ya teknolojia duniani.

Aidha amewahimiza watangazaji na waandishi wa habari kwa jumla hapa Zanzibar, kujifunza zaidi matumizi ya vifaa vya kisasa pamoja na lugha za kigeni ili waweze kujifungulia milango ya kukubalika kwenye Idhaa mbalimbali duniani zinazotangaza kwa lugha ya Kiswahili ikiwemo DW.

“Huu si wakati wa kufanya kazi kienyeji, ni lazima mchangamkie fursa kama hizi kwa kujibidiisha kazini na kutumia vyema nafasi za mafunzo zinazopatikana ndani na nje ya nchi. Elimu ndio ufunguo wa kukupaisheni,” alisisitiza Waziri huyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Ujerumani Bibi Andrea Schmidt, amesema pamoja na fursa nyingi za mafunzo na utangazaji zinazotolewa na idhaa hiyo, lakini ni muhimu watangazaji kujiendeleza katika lugha nyengine  za kigeni.

Alifahamisha kuwa, uwezo katika lugha za kigeni ikiwemo Kingereza, ni miongoni mwa vigezo vya msingi ili mtangazaji aweze kufanya kazi katika idhaa hiyo iliyoko Bonn nchini Ujerumani.

Alieleza kuwa, Idhaa hiyo iliyotimiza miaka 55 tangu kuanzisha matangazo kwa lugha ya Kiswahili, inaendelea kutoa nafasi kwa watanzagaji wa Zanzibar, ambapo mwezi Februari mwakani, wanatarajia kupokea mtangazaji mmoja kutoka miongoni mwa redio binafsi za hapa nchini.

Hata hivyo, alisema vyombo vya habari havipaswi kusimama vilipo kwa kuendelea kutangaza kizamani, bali ni lazima viangalie mahitaji ya wakati wa sasa na nini wasikilizaji wao wanapenda.

“Maendeleo ya vyombo vya habari hayategemei tu vifaa vya kisasa, bali muhimu zaidi kuzifanya redio zivutie watu kwa kuangalia nini wanapenda kusikia miongoni mwa mambo mbalimbali ya kijamii, kisiasa, burudani na maendeleo,” alifafanua.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara anayeshughulikia habari Dk. Saleh Yussuf Mnemo na Mshauri wa Waziri Abdalla Mwinyi Khamis, walisema ujio wa Mkuu huyo ni fursa nyengine ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa nchi zao katika tasnia ya habari.

Mkuu huyo aliambatana na mtangazaji mstaafu wa Idhaa hiyo kutoka Zanzibar Ramadhan Ali, aliyekitumikia kituo hicho kwa miaka 41 akitokea iliyokuwa Sauti ya Tanzania Zanzibar, sasa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).

Na Salum Vuai, WHUMK