Mamlaka ya anga, wazungumzia ‘perfume’ zinazoachwa na abiria Airport

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini (TCAA) imesema marashi yote ambayo abiria wamekuwa wakizuiwa kuingia nayo kwenye ndege huteketezwa kila siku chini ya uangalizi wa polisi.

Akiwasilisha mada  ya masuala ya kiusalama yanayopaswa kuzingatiwa na abiria wa usafiri wa anga katika mafunzo kwa waandishi wa habari leo Juni 11 2018, Inspekta Mwandamizi wa Usalama wa Usafiri wa Anga (TCAA) Salim Msangi amesema  uteketezaji hufanywa kila jioni katika viwanja vya ndege nchini chini ya usimamizi wa polisi.

“Kuna watu wamekuwa wakisema tunanyang’anywa perfume (marashi) wanaenda kuzitumia. Nataka niwahakikishie kuwa hakuna mtu anayechukua perfume za mtu,”amesema.

Amesema watu kuzuiwa kuingia kwenye ndege na marashi kunatokana na kutokuwapo kwa mashine inayoweza kugundua kama marashi husika yanaweza kutumika kama mlipuko.

Amesema kuwa marashi yanayoruhusiwa ni yenye ujazo usiozidi milimita 100 na wale wenye ujazo unaozidi kiasi hicho basi wanapaswa kwenda katika mizigo inayokwenda chini ya ndege.

Kuhusu ukaguzi kwa watu mashuhuri, Msangi amesema kwa mujibu wa mkataba wa 1969 wa Vienna, watu wote wanaosafiri kwa kutumia ndege hawana kinga ya kutokaguliwa.