Waziri: Wanahabari msivae gwanda kisiasa

VITUO vya habari vinavyoendelea kuanzishwa visiwani Zanzibar, vimeshauriwa kutoegemea upande wowote kisiasa vinapotoa habari zao hasa katika vipindi vya uchaguzi.

Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo, amesema serikali inavipa leseni vyombo hivyo ili visaidie kuielimisha jamii juu ya mambo mbalimbali ya maendeleo na umuhimu wa kuendeleza amani iliyopo nchini.

Akizungumza na uongozi na wafanyakazi wa TIFU TV alipotembelea kituo hicho Vikokotoni mjini Zanzibar, Waziri Kombo alisema, vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kudumisha amani iwapo vitaepuka kutoa taarifa zinazofarakanisha watu.

Hata hivyo, alisema iwapo vitakengeuka maadili na miko ya tasnia ya habari, vinaweza kuwa chanzo cha kutoweka amani na usalama, akitoa mfano wa nchi za Rwanda, Burundi na baadhi ya mataifa ya Afrika Kaskazini yaliyosambaratika kutokana na kalamu za waandishi wa habari zilizotumiwa vibaya.

“Wakati wa uchaguzi bakieni kwenye kazi yenu ya kuwapasha habari wananchi kuhusiana na yanayoendelea kwa usahihi bila kutia chumvi wala kupendelea upande wowote, siasa tuachieni sisi wanasiasa,” alisisitiza.

Aidha alivikumbusha vyombo vya habari vya serikali na binafsi, kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kushiriki kwa kujitolea kizalendo katika ujenzi wa nchi yao, na kuhubiri umoja na mshikamano.

Waziri Kombo alisema mwandishi au chombo cha habari kizuri ni kile kinachohakikisha uandishi na vipindi vyake vinahamasisha kuwaleta pamoja watu badala ya kuwafarakanisha.

Alifahamisha kuwa yapo mambo mengi ambayo wananchi wanapaswa kuelezwa kupitia vyombo vya habari, kama vile utunzaji mazingira na afya ya jamii ili kuiepusha nchi na maradhi yakiwemo ya mripuko, masuala ya udhalilishaji na vita dhidi ya dawa za kulevya.

Halikadhalika, aliviagiza vyombo hivyo kuyatangaza  maeneo ya kihistoria na mambo ya kale kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi ili waone umuhimu wa kuyatembelea badala ya kuwaachia watalii kutoka ng’ambo peke yao.

Halikadhalika, aliitaka TIFU TV na vituo vyengine vinavyorusha habari mitandaoni (Online Reporting), kuhakikisha taarifa zao zinafanyiwa utafiti wa kina unaotoa haki kwa pande zote ili kujiepusha na migogoro inayoweza kuzilazimisha mamlaka kuvifungia.

Hata hivyo, alikipongeza kituo hicho kwa jitihada zake za kuifikia jamii, akiwasifu wafanyakazi wake kwa namna walivyo wepesi kuyafuata na kuyaripoti matukio yanayowagusa wengi mara wanapopata taarifa.

Naye Mkurugenzi wa TIFU TV Abdalla Keisy, alimshukuru Waziri huyo kwa kuvijali vyombo vote vya habari, akisema utendaji wake unaonesha wazi kuwa anapenda kuona tasnia ya habari inayokabiliwa na ushindani mkubwa inafika mbali.

Alisema kituo chake kipo kuwasaidia wananchi ambao sauti zao si rahisi kusikika hasa pale wanapokuwa na matatizo ya kijamii, na ndio maana wakachagua kaulimbiu (Motto) iitwayo ‘Kijamii zaidi’.

Alimuhakikishia Waziri huyo na serikali kwamba kadiri kituo chao kinavyokua, wataendelea kufuata sheria namiongozo yote inayosimamia vyombo vya habari kwa manufaa ya sasa na baadae.

 

WAZIRI wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo, akioneshwa jinsi matangazo ya televisheni katika kituo cha TIFU TV yanavyorushwa hewani alipofanya ziara kuangalia shughuli za kituo hicho. Kulia ni Mkurugenzi Abdalla Keysi, na kushoto aliyesimama ni mmiliki Abdullatif Masoud Salum. (Picha na Salum Vuai, WHUMK).

 

WAZIRI wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo (Kulia), akimsikiliza Mkurugenzi wa TIFU TV Abdalla Masoud Salum alipofanya ziara kuangalia shughuli za kituo hicho.

 

Na Salum Vuai, WHUMK