Taarifa rasmi kuhusu sherehe za Mwaka Kogwa 2018

Mkuu wa mkoa Kusini Unguja Mhe. Hassan Khatib Hassan amesema Serikali mkoani humo itahakikisha inafanya kila iwezalo ili kuona kwamba sherehe za kijadi za Mwaka Kogwa kwa mwaka huu zinafanikiwa kama zilivyopangwa.

Mkuu wa mkoa Kusini Unguja Mhe. Hassan Khatib Hassan

Mhe. Khatibu ameyasema hayo katika ofisi ya mkuu wa wilaya  Makunduchi wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa vyombo mbali mbali vya habari na wazee wa mwaka kongwa pamoja na wajumbe wa kamati ya usalama ya mkoa juu ya mipango ya maandalizi ya sherehe hizo.

Amesema sherehe hizo ambazo huwa zinaadhimishwa kila mwaka ktk kijiji cha Makunduchi kwa mambo mbali mbali ya kijadi imekua kivutio kikubwa kwa wageni wa ndani na nje ya nchi ambapo amewataka wana Makunduchi na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya Zanzibar kuungana katika kusherehekea siku hio..

Amefahamisha kwamba sherehe hizo mbali ya kivutio lakini pia imeweza kuitangaza na kuipatia umaarufu Zanznibar katika nchi mbalimbali Barani Afrika na nyenginezo ulimwenguni sambamba na kukuza ustawi wa uchumi hasa katika sekta ya utalii.

Akizungumzia kuhusu masuala ya udhalilishaji  katika sherehe hizo mkuu huyo amesema serikali itachukua hatua madhubuti ya kudhibiti vitendo hivyo ikiwemo wa kuweka muda maalum kwa matumizi ya fukwe, ambayo ni maeneo yenye ushawishi mkubwa wa vitendo mbali mbali vikiwemo vya udhalilishaji.

Nae Kamanda wa Polisi kamishna msaidizi wa Polisi  mkoani humo Suleiman Hassan Suleiman  amesema jeshi la polisi limejipanga vyema  katika kuimarisha usalama kwenye maeneo yote ikiwemo barabarani, kiwanja cha skukuu na maeneo ya fukwe pamoja na raia na mali zao na kuonya kwamba iwapo atatokea mwananchi kujaribu kuvunja amani hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Nao wazee wa Mwaka Kogwa kwa upande wao wamesema wanaendelea kuadhimisha  sherehe  hizo za kijadi walizorithi kutoka kwa wazee wao  kwa kufanya mambo mbalimbali ya kimila ikiwemo matambiko na kuomba amani ya nchi kwa kuepukana na majanga maradhi , ajali, njaa na mafuko.

Sherehe hizo za Mwaka Kongwa zitafanyika tarehe 18 mwezi huu ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim  Majaliwa.

Rauhiya Mussa.