RC Kusini Unguja awaasa wazazi kutowaozesha watoto katika umri mdogo

Mkuu wa mkoa wa Kusini Unguja Mhe. Hassan Khatib Hassan amewataka wazazi na walezi mkoani humo kuacha tabia za kuwaozesha watoto wao katika umri mdogo na badala yake kuwashajihisha katika suala zima la kujiendeleza kielimu.

Mhe. Hassan ameyaeleza hayo Skuli ya Sekondari Jendele wakati alipokuwa akiwakabidhi  zawadi wanafunzi wa kidatu cha kwanza hadi cha nne ambao wamefanya vizuri katika mitihani yao ya  muhula na wanafunzi watatu ambao wamefaulu kuingia kidato cha tano mwaka jana kwa skuli hiyo.

Amesema umefika wakati kwa wazazi kuona umuhimu wa kuwaendeleza watoto wao hasa wa kike kwani ndio njia pekee itakayowawezesha kuwajengea mustakbali mzuri wa maisha yao ya baadae.

Aidha amesema kwamba kumuelimisha mtoto wa kike kielimu ni sawa na kuielimisha jamii nzima kwani watoto wa kike wanapata nafasi kubwa ya kuwa karibu na jamii  na kuwa na uwezo mkubwa wa uwajibikaji katika nafasi za uongozi katika sekta za Umma na binafsi.

Hata hivyo Mhe. Hassan amewasisitiza wanafunzi hao kuzidisha bidii katika masomo na kujiepusha na vishawishi hatarishi ambavyo vitapelekea kuharibu masomo yao sambamba na kuwataka walimu kutotosheka na elimu waliyokuwa nayo na badala yake kujiendeleza zaidi ili kuweza kupata mbinu bora za ufundishaji.

Katika risala yao wanafunzi hao wamesema licha ya mafanikio wanayoyapata lakini bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo za kutokuwa na uzio katika eneo lao la skuli, ukosefu wa mashine ya fotokopi pamoja na maabara jambo ambalo linapelekea usumbufu kwa walimu na wanafunzi katika kujifunza.