Wabunge Kenya waumbuliwa kuhudhuriwa kombe la dunia kimya kimya

Raia wa Kenya wamewajia juu wabunge baada ya kubainika kuwa watunga sheria hao wamesafiri kwenda kuhudhuria Fainali za Kombe la Dunia Urusi wakitumia fedha za walipa kodi licha kwamba taifa lao halikufuzu kushiriki michuano hiyo.

Sakata hilo liliibuka baada ya wabunge hao kutumia picha za selfi katika mitandao ya kijamii wakifurahia kutazama mechi za soka nchini Urusi.

“ Haya ni masihara mabaya kabisa …yaani viongozi wanasafiri hadi Urusi kwa ajili ya kuangalia soka wakati tunakabiliwa na matatizo mengi,” alihoji Sylvester Aseka anayejishughulisha na uuzaji wa kompyuta zilizotumika.

“Mungu wangu nataka niamini kuwa jambo hili siyo kweli kuhusu picha ambazo baadhi yao wamekuwa wakizituma,” alisema Jacinta Mong’ina ambaye ni mwanafunzi na kuongeza: “ Inamaanisha wana fedha nyingi na muda wa kutosha kwenda Urusi. Lini watayatumikia majimbo yao?”

Gazeti la The Star daily limeripoti kuwa karibu wabunge 20 walisafiri mwanzoni mwa mwezi huu kwenda Urusi kuhudhuria michuano ya Kombe la Dunia na wanatarajia kuwepo huko hadi michuano hiyo itakapomalizika.