Kamati ya Utendaji ya Taifa ya THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi) imekutana katika kikao cha dharura cha siku moja leo hii katika Makao Makuu ya Chama, mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama, Maalim Seif Sharif Hamad.

Kikao hicho kilikuwa na ajenda moja tu ambayo ni Maandalizi ya Uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi za Madiwani 22 kwa upande wa Tanzania Bara na nafasi ya Ubunge wa jimbo la Dimani kwa upande wa Zanzibar.
Kamati ya Utendaji ya Taifa imepitisha ratiba ya uchaguzi wa ndani ya Chama kwa ajili ya kuwapata wagombea wa CUF katika nafasi hizo ambayo itasambazwa katika Wilaya na Kata husika kufuatia kukamilika kwa kikao hiki.

Ikumbukwe kwamba CUF bado ni sehemu ya UKAWA na suala hilo lilipitishwa na Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama uliofanyika 23 – 27 Juni, 2014 ambacho ndicho chombo cha juu kabisa na chenye maamuzi ya mwisho katika Chama. Kwa msingi huo, hakuna mtu yeyote mwenye uwezo wa kutengua uamuzi huo isipokuwa Mkutano Mkuu wa Taifa wenyewe tu. Kwa sababu hizo, CUF inaendelea na mazungumzo na vyama vyengine vinavyounda UKAWA kuona namna bora ya kushiriki chaguzi hizi itakayohakikisha kuwa tunaibwaga CCM.

Katika hatua nyengine, Kamati ya Utendaji ya Taifa imeshangazwa na kauli ya ajabu ya Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ndugu Ramadhani K. Kailima, kusema kwamba wagombea wa CUF katika uchaguzi huo ni lazima fomu zao za uteuzi zithibitishwe na kutiwa saini na Yule aliyemwita Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na Katibu Mkuu wa Chama, na kwamba kinyume na hivyo, wagombea hao hawatotambuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Kauli hii ya Ndugu Kailima inathibitisha kwa mara nyengine kwamba vyombo na taasisi za Dola vinatumika kikamilifu kupandikiza na kuchochea ule unaoitwa mgogoro ndani ya CUF kwa lengo la kukihujumu Chama chetu. Masuala ya uteuzi wa wagombea na fomu za uteuzi wa wagombea yanaongozwa na Sheria ya Uchaguzi na Kanuni za Uchaguzi.

Ndugu Kailima amekitoa wapi kifungu cha Sheria au Kanuni alichokitumia kuweka sharti hilo la ajabu tena kwa chama kimoja tu? Mojawapo ya misingi ya sheria ni kutokuwepo kwa ubaguzi katika utungaji na utekelezaji wa sheria. Huwezi kuwa na sharti linalokihusu chama kimoja tu katika kuthibitisha uteuzi wa wagombea .

Masuala ya jinsi ya kuwapata wagombea wa Chama yanayongozwa na Katiba ya Chama ya 1992 (Toleo la 2014) na Kanuni za Uchaguzi wa ndani ya Chama.

Fomu za uteuzi wa wagombea kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi siku zote huthibitishwa na Katibu wa Chama wa ngazi inayohusika na kwa Ubunge na Madiwani imekuwa ni Katibu wa Wilaya. Kitendo cha Ndugu Kailima kuja na sharti lake kutoka mfukoni kuihusu CUF katika chaguzi hizi ndogo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi na ni mwendelezo wa hujuma za Dola na taasisi zake dhidi ya CUF kwa kumtumia mtu anayeitwa Ibrahim Lipumba. CUF haitozikubali hujuma hizi na itazilinda na kuzitetea haki zake za kikatiba na kisheria kikamilifu.

Mwisho kabisa, Kamati ya Utendaji ya Taifa inawapongeza wanachama wa CUF kwa ujasiri wao wa kukilinda Chama chao kwa mapenzi na nguvu zao zote dhidi ya njama za wanasiasa muflisi ambao wamekubali kujiuza kwa bei rahisi kutumikia watawala wakidhani wanaweza kukivuruga Chama hiki.

Kamati ya Utendaji ya Taifa inawahakikishia wanachama wote wa CUF kwamba iko imara na itaendelea kufanya kazi ya kukilinda na kukitumikia Chama na wajue kwamba tutashinda MAPAMBANO HAYA.

HAKI SAWA KWA WOTE

Kamati ya Utendaji ya Taifa
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi)
13 Desemba, 2016