Yanga leo wamefanikiwa kutinga hatua ya 16 bora baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-1, dhidi ya Ashanti United Kombe la FA.

Mabingwa watetezi wa kombe la FA, Yanga leo wamefanikiwa kutinga hatua ya 16 bora baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-1, dhidi ya Ashanti United katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Katika mchezo huo mabao ya Yanga yalifungwa na Amissi Tambwe, Thabani Kamusoko, Simon Msuva na Yusuph Mhilu aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Tambwe huku lile la Ashanti likifungwa na Sharif Mohammed.

Licha ya ushindi huo mnono Yanga leo haikuweza kuwatumia nyota wake muhimu wa kikosi cha kwanza akiwemo kipa Deogratius Munishi ‘Dida’, Kelvin Yondani, Haruna Niyonzima na Donald Ngoma waliopumzishwa kwa ajili ya mechi zijazo za Ligi Kuu.

Yanga walikwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao mawili yaliofungwa na Tambwe aliyefunga bao la kwanza dakika ya 19 na Kamusoka alifunga la pili kwa shuti kali la mbali dakika ya 36.

Ashanti walijitahidi kupambana ili angalau kupata bao moja lakini washambuliaji wake walionekana kukosa maarufa ya kuwapenya mabeki wa Yanga.

Mshambuliaji wa Ashanti Rajabu Mohamed alijaribu kuwapangua wabeki wa Yanga dakika ya 41 lakini shuti lake halikuweza kulenga lango na mpira kutoka nje.

Kipindi cha pili Yanga walikianza kwa kasi na katika dakika ya 52 walifanikiwa kufunga bao la pili kupitia kwa Msuva, aliyefunga kwa penati baada ya yeye mwenyewe kuangushwa na Suleimani Sultani akiwa ndani ya eneo la hatari.

Mchezo huo uliendelea kwa Ashanti kuonekana kutawala eneo la kiungo na kutengeneza nafasi nyingi ambapo dakika ya 62 Mohammed aliifungia timu yake bao la kufuatia Endrew Vicent wa Yanga kujichanganya na kumwachia mpira mfungaji.

Baada ya kufungwa bao hilo Yanga waliendelea kupambana na dakika ya 89 Mhilu aliifungia timu yake ya bao la nne na kuipeleka hatua ya 16 kwa ushindi mono wa mabao 4-0.

Kwa matokeo hayo sasa Yanga itasubiri kupangiwa timu itakayokutana nayo kwenye hatua hiyo baada ya kumalizika mechi zote za hatua ya 32 ambazo zitachezwa hadi kesho Jumatatu.

 

Chanzo: Goal