Watu 36 wamefariki katika mgodi mmoja siku ya Alhamisi baada ya upande mmoja wa mgodi huo wa shaba kuporomoka kusini mashariki mwa Congo, kulingana na gavana wa mkoa huo.

Ajali hiyo ilitokea katika shimo la mgodi huo wa kampuni ya Kamoto Copper Company KCC , ambayo ni kampuni tanzu ya kampuni kubwa ya uchimbaji madini duniani Glencore yenye umiliki wa asilimia 75 ya hisa zake alisema Richard Muyej Gavana wa mkoa wa Lualaba.

”Ajali hiyo ilisababishwa na wachimbaji haramu waliovamia mgodi huo”, aliambia shirika la habari la Reuters, hatua hiyo ilifanya eneo moja la mgodi huo kuporomoka katika shimo hilo.

”KOV ni eneo linaloweza kuharibika kwa urahisi na ni hatari”, aliongeza.