MAMLAKA ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar ZAECA afisi ya Pemba, imemtia mikononi mtendaji mmoja wa Baraza la mji la Wete kisiwani Pemba, baada ya kudakwa akipokea rushwa ya shilingi 290,000 kati ya shilingi milioni 2.5 alizoziomba kwa mlalamikaji.

Taarifa za ZAECA zilizonaswa na mwandishie wetu zinaeleza kuwa, mtendaji huyo alimuomba rushwa mtu mmoja ambae alimuahidia kumpa nafasi ya ajira, ndipo alipotoa taarifa hizo ZAECA.

Imefahamika kuwa, baada ya mwananchi huyo kuiarifa Mamlaka hiyo, ndipo watendaji hao walipotega mtego kwa kushirikiana na mwananchi huyo, kisha mtendaji huyo kunaswa.

Mara baada ya kukamatwa akipokea kiasi cha shilingi 290,000 alichukuliwa na watendaji hao wa ZAECA, hadi makao makuu mjini Chakechake na kuhojiwa kwa takriban saa moja, huku akikubali kupokea fedha hizo.

Imeelzwa kuwa, mtendaji huyo wa baraza la mji wa Wete, alisema hakupokea fedha hizo kwa ajili ya kumpatia ajira mlalamikaji huyo kama alivyoeleza, bali ni kwa ajili ya mambo mengine.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mkurugenzi mkuu wa ZAECA Zanzibar Mussa Haji Ali, alikiri kumshikilia mtendaji huyo, na kusema taratibu zikikamilika jalada la kesi yake litafikishwa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ‘DPP’.

“Ni kweli yupo mtendaji wa Baraza la mji wa Wete, tumemshika akipokea rushwa ya shilingi 290,000 kati ya shilingi milioni mbili  na laki tano (2,500,000) alizoomba kwa muhusika, na tumeshamuhoji’’,alisema.

Alisema wao baada ya kumshikilia mtu kwa madai ya rushwa, huandaa jalada la kesi na kulifikisha mbele ya afisi ya DPP na kuangalia iwapo kuna kesi dhidi ya mtuhumiwa.

Aidha Mkurugenzi huyo alisema, taarifa zilizorahisisha kukamatwa kwa mtendaji huyo wa baraza la mji Wete, ni kufuatia mwananchi aliedaiwa rushwa, kuamua kutolifumbia macho suala hilo na kuamua kuwapa taarifa watendaji wake.

“Mfano wa mwananchi huyu ndio haswa ZAECA inayowataka wananchi kutoa taarifa, wanapohisi wanataka kuuziwa haki zao, kama ajira hakuna haki ya kutoa fedha’’,alifafanua.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mtendaji huyo wa Baraza la mji wa Wete kisiwani Pemba kwa masharti ya kutajwa jina lake, alisema inaonyesha dhahiri mpango huo ni kuwapangwa.

“Mimi sina ahadi na mwananchi yeyote kwamba anitafutie fedha ili nimuajiri, mimi nimepokea fedha lakini hatuna mipango ya kumuajiri, bali ni mpango wa makusudi wa kuniangusha kwenye kazi yangu”,alilalamika.

Alieleza kuwa, amekuwa akipokea taarifa mbaya mbaya za baadhi ya wafanyakazi wenzake, hasa kutokana na kufanya kazi zake kwa kufuata sheria, na kanuni.

“Mimi nahisi baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakinichukia kutokana na kufanyakazi zangu kwa mujibu wa sheria, sasa inawezekana wao wameshazoea kuvuruga kwenye kazi’’,alieleza.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wa habari hizi, wameitaka ZAECA kuendelea na kazi zake, ili kuhakikisha wanyonge wa nchi hii, nao wanaendelea kupata haki zao kwenye taasisi za umma.

Ali Muhisin Makame wa Machomane Chakechake, alisema elimu ya kujielewa wananchi nafasi yao katika kupinga rushwa, lazima iendelee kutolewa na ZAECA.

Nae Asha Mbaraka Muhidin wa Wawi alisema, lazima jamii iisaidie sana ZAECA, ili ifanikishe kazi zake za kupambana na wanaotumia vibaya mamlaka na nafasi zao, kwenye taasisi.

Kwa mujibu wa sheria ya ZAECA no 1 ya mwaka 2012 kwenye kifungu cha 61 kinaeleza kuwa iwapo, mtu atatiwa hatiani kwa kosa la rushwa, ni kifungo kisichopungua mika miwili jela na kisichozidi miaka mitano, au faini ya isiopungua shilingi milioni mbili au isiozdi shilingi milioni tano au vyote kwa pamoja.

ZAECA kwa kisiwani Pemba pekee, inaendelea kufanya uchunguuzi wastani wa matukio 20 ya kesi za rushwa za aina mbali mbali zailizowasilishwa afisini hapo, wakati tayari kesi moja kwa sasa, iko mahakamani ikiendelea na taratibu.