Ongezeko kubwa la talaka limeanza kuwashituwa jamii na hata baadhi ya viongozi wa dini kisiwani  Pemba baada ya kugunduliwa  kuwa vijana wengi wanatoa talaka kiholela bila  ya kuzingatia maelekezo wanayoyapata wakati wa kufunga ndoa  pamoja na misingi mikuu ya dini yao ya kiislamu inavyotaka wakati wa kutoa talaka pale inapobidi.

Miongoni mwa wanazuoni iliyawashituwa hali hiyo ni pamoja na fadhilat sheikh Abdulirahman Abdallah Naaman msaidizi katibu wa mufti Pemba.  Akizungumza na bustani ya habari Sheikh Naaman alionyesha kukerwa na jinsi vijana wanavyotoa talaka kiholela bila ya kuzingatia maelekezo wanayopata kutoka kwa mashehe zao wakati wa kufunga ndoa.

Shekh Naaman amesema kuwa vijana wengi hawazingatii elimu ya ndoa na badala yake pale wanapopata matatizo ndani ya ndoa huona suluhisho ni kutoa talaka jambo ambalo ni kinyume na utaratibu wa misingi ya ndoa.

Kufuatia hali hiyo msaidizi katibu huyo amesema hali hiyo haiwezi kuachiwa iendelee na badala yake ofisi yake ikishirikiana na mahakama za kadhi zinapanga mipango madhubuti itakayoweza kupunguza talaka za kiholela na kuwafanya vijana wengi kudumu katika ndoa zao.

Aidha msaidizi katibu huyo amekemeaa utolewaji wa talaka tatu ambazo mtu hawezi tena kurejea na baadae mtu hupanga kutolewa muhalili ni kosa na kusema jambo hilo katika dini halipo ..

Kwa upande wao  badhi ya wazee kisiwani Pemba wakizungumzia jambo hili la talaka za kiholela wao wameona kutokuwa na subra na uvumilivu kwa wana ndoa wa leo ndio chanzo kikuu cha utolewaji wa talaka za kiholela.

Hivyo wamewataka wazazi wenzao kukaa chini na vijana wao kuwapatia mafunzo ambayo yatawasaidia kudumu katika ndoa zao.